Akisoma maoni ya Kamati ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka 2016/17, Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Vicky Kamata alisema hawaridhishwi na namna Serikali inavyotoa fedha za bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“Kwa kuzingatia takwimu hizi ni dhahiri miradi mingi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha haitatekelezwa,” alisema Kamata.
Alisema kamati hiyo inaunga mkono dhamira ya Serikali ya kuifanya nchi kuwa ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025 lakini hairidhishwi na kasi ya utekelezaji wa azma hiyo.
“Hali hii ikiendelea itakuwa vigumu Tanzania kuwa nchi ya viwanda iwapo Serikali itaendelea kuchelewesha utekelezaji wa miradi yenye mchango mkubwa katika sekta hii,” alisema.
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu alisema: “Kamwe tusijiaminishe kuwa tunaweza kufikia Taifa la viwanda kwa Sh42.159 bilioni kwenye bajeti ya mwaka kama fedha za maendeleo kwa ajili ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,” alisema.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni jana Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema kati ya viwanda 106 vilivyofanyiwa tathmini, viwanda 45 vinafanya kazi, 24 vinasuasua na 37 vimefungwa.
“Mpango wetu ni kuhakikisha kuwa viwanda 35 vilivyobaki vinafanyiwa tathmini haraka na kabla ya nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha unaoanza Julai Mosi mwaka huu, hatima ya viwanda visivyofanya kazi itajulikana,” alisema.
Alisema hatima ya wenye viwanda visivyofanya kazi ni kwa wamiliki kutekeleza mkataba ya mauzo au kupewa wawekezaji wapya ili waviendeleze,” alisema.
Wizara hiyo imeomba kutengewa Sh 81.87 bilioni katika mwaka wa fedha 2016/17 kati ya hiyo, Sh41.87 bilioni sawa na asilimia 51 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh40 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Post a Comment