Dar es Salaam. Picha za watu wa kada mbalimbali nchini wakiigiza ‘staili’ mpya ya wabunge wa Ukawa waliojibandika karatasi midomoni zenye ujumbe tofauti kuhusu haki ya uhuru wa Bunge wanayodai kuminywa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson zimeiteka mitandao ya kijamii nchini.
Tukio la wabunge hao lilitokea juzi mjini Dodoma ikiwa ni mwendelezo wa siku 17 za kususa vikao vinavyoongozwa na Dk Tulia tangu akatae kujadili hoja ya kusimamishwa wanafunzi 7,802 wa stashahada maalumu ya sayansi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), wiki tatu zilizopita.
Kama ilivyokuwa kwa wabunge hao, watu mbalimbali wanapiga picha za kuigiza tukio hilo na kuziweka katika mitandao ya facebook, twitter na Instagram, baadhi wakiandika ujumbe kwenye karatasi wanazobandika midomoni ama wakiwaponda Ukawa au wakiwaunga mkono.
Mbali na waliobandika karatasi midomoni, wengine waliamua kujiziba kwa nguo, vilemba huku baadhi wakitumia kadi za CCM na Chadema na kuweka ujumbe wa kukosoa au kupongeza tukio hilo huku wengine wakitumia neno ‘kuziba mdomo’ kutoa yao ya moyoni ambayo hayahusiani na kitendo cha wabunge wa Ukawa.
Tukio hilo lilivuta wafuatiliaji wengi katika mitandao hiyo, katika ukurasa wa facebook wa gazeti hili @MwananchiNews, watu 255,372 walifungua picha za wabunge hao wa Ukawa huku watu 922 wakizinakili na kuzituma katika kurasa zao za mtandao.
Mbali na kuzifuatilia, wengine kwa mamia walikuwa wakitoa maoni yao yakieleza hisia mbalimbali.
Hali kama hiyo pia ilijitokeza katika tovuti ya Milladayo ambako watu 255 walitoa maoni yao katika picha hizo huku wakilumbana vikali.
Mkazi wa Dar es Salaam, Hilda Newton katika ukurasa wake wa facebook aliweka picha yake iliyoambatana na ujumbe unaosema ‘mkuu wa kaya acha kutuziba midomo na kukandamiza uhuru wa kuongea’.
Shija Steven katika ukurasa wake wa mtandao huo wa kijamii aliweka picha ya wabunge hao na kuponda kitendo walichokifanya, huku akiwashauri kwenda majimboni kutatua matatizo yanayowakabili wananchi.
Evelyne Ngoyai Meena katika ukurasa wake wa facebook aliandika, “kama mnafanya mambo mazuri kwanini hamtaki watu waongee, uhuru wa kujieleza uko wapi? Yanayoendelea nchi hii ni sawa na kufanya mtihani halafu unataka ujisahihishie mwenyewe.”
Picha za mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa katika ukurasa wake wa facebook zinazowaonyesha wabunge hao, zilijadiliwa na watu 7,971 huku watu 822 wakizinakili na kuziweka katika kurasa zao.
Katika ukurasa wake wa twitter, Papa Mchoyo aliweka picha ya mtu aliyejiziba mdomo kwa karatasi iliyoandikwa, “wabunge Ukawa achene maigizo.”
Kwa upande wake, Rev Mimba katika mtandao wa twitter aliandika, “tusiwabeze wabunge wa upinzani kuziba midomo katika political tactics (mbinu za kisiasa) za kufikisha ujumbe mbali na hiyo ni mojawapo.
Post a Comment