Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa, waliohojiwa jana, walisema kitendo hicho ni mkakati usio na tija huku wengine wakisema ni maoni ya kujifurahisha. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema kitendo hicho cha Zitto ni ‘mkakati usio na tija’. Naibu Katibu wa Bunge, John Joel alisema ‘ni maoni ya kujifurahisha’ wakati Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba alisema atajitokeza hadharani baadaye kutoa maoni ya kuliunganisha Taifa.
Baada ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge hivi karibuni kutokana na kukiuka taratibu, Zitto amekuwa akitumia majukwaa kukosoa bajeti na Serikali ya Rais John Magufuli, hatua ambayo imeelezwa pia kuwa inashusha heshima ya Mbunge huyo. Warioba kufunguka Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, alipotakiwa kutoa maoni yake kwa hatua hiyo, alisema wakati utakapofika atajitokeza na kueleza namna wanasiasa wanavyotumia vibaya nafasi zao za kisiasa.
“Kwa sasa tumekaa kimya, lakini wakati utafika ambapo tutajitokeza na kutoa maoni yetu kwa maslahi mapana ya taifa pamoja na kwamba tunaona namna wanasiasa wanavyotumia vibaya nafasi zao za kisiasa na kuligawanya Taifa. Kazi yetu sisi ni kuliunganisha taifa kuwa moja,” alisema Jaji Warioba.
Mhadhiri amshangaa Zitto Kwa upande wake, Dk Bana akizungumza na gazeti hili jana alisema; “ Zitto alipaswa kukusanya maoni ya wananchi ili kuyapeleka bungeni.” “Wakati serikali ilipokuwa inaandaa bajeti yake ya mwaka huu na hata Mpango wa Taifa wa Maendeleo, Zitto alipata fursa ya kushiriki maandalizi yake katika hatua mbalimbali akiwa Mbunge.
“Ni wakati huo ndipo Zitto alipaswa kukusanya maoni ya chama chake au makundi mengine ya kijamii wakiwemo wananchi wake ili baadaye ayawasilishe serikalini au bungeni ili kuwezesha kupatikana kwa bajeti bora na si hatua hii anayoichukua sasa,” alisema Bana.
Alisema Mbunge huyo pamoja na kuzijua fika taratibu za Bunge, aliamua kwa makusudi kuzikiuka na hivyo kupoteza dhamana aliyokabidhiwa na wananchi ya kuwawakilisha ndani ya Bunge ili kujadili masuala yenye maslahi mapana kwa taifa ikiwemo bajeti na sasa amebuni mkakati usio na tija.
Alisema pamoja na kufahamu umahiri wa mbunge huyo katika medani ya siasa hatua ambayo iliwezesha wananchi kuwa na imani kubwa na mustakabali wake kisiasa, kwa bahati mbaya Mbunge huyo amepoteza mwelekeo na kuanza kutoa kauli alizosema hazina manufaa kwa wananchi.
“Anachoendelea kukifanya Zitto ni mwendelezo wa kile alichokifanya Mbagala alipotoa lugha ya kuudhi dhidi ya Rais (John Magufuli). Wote tunajua mambo ya bungeni yanajadiliwa bungeni. “Haiwezekani leo mwanasiasa anayejiita mahiri anaitisha mjadala kuhusu bajeti wakati hotuba ya bajeti ikiwa mezani na wananchi wakifuatilia mjadala wake bungeni, huku ni kuwavuruga wananchi na si jambo la msingi kwa taifa,” alisema Profesa Banna.
Akizungumzia mwelekeo wa kisiasa kwa Mbunge huyo wa Kigoma Mjini, Bana alisema pamoja na kuaminiwa kuwa na sauti yenye ushawishi na mvuto wa kisiasa, lakini wasomi wamekuwa wakimchukulia Zitto kama mwanasiasa anayeanzisha hoja na kuziacha hewani bila kuzimaliza.
“Ni tofauti na Kafulila (David- Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini). Zitto anapenda kuanzisha hoja na kuziacha zikielea. Kila siku anakuja na hoja mpya, mara bajeti, mara fedha zilizofichwa nje, mara Escrow, mara rais hivi. Ni mtu ambaye hoja zake zinafichwa na ajenda binafsi nyuma yake,” alisema Bana.
Ofisi ya Bunge yafafanua Kwa upande wake, akitoa maoni kuhusu msimamo wa Bunge kwa hatua hiyo ya Mbunge Zitto kuhamishia mjadala wa bajeti nje ya Bunge, Naibu Katibu wa Bunge , John Joel alisema pamoja na kuwa kitendo hicho hakizuiliwi, lakini hakina tija kwa wananchi.
“Zitto anaendesha mjadala ili apate maoni ya kumpelekea nani?” Alihoji Joel na kusema kuwa Mbunge huyo angeweza kukubalika zaidi endapo angetumia jukwaa la Bunge kujadili kile anachokiona katika bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha.
Naibu Katibu huyo wa Bunge alisema kinachoshangaza zaidi ni kuona kuwa mkakati huo wa kujadili bajeti, hata pale unapoonekana kuvalishwa joho la chama cha ACT – Wazalendo ambapo Zitto ni Kiongozi Mkuu, lakini haufanywi kwa vikao vya ndani vya chama na badala yake unaelezwa kuwa ni mjadala wa wazi, hatua inayochanganya wananchi.
Post a Comment