ZAIDI ya Watanzania 500 walioko nchini India pia nchi nyngine wameomba msaada wa kurejeshwa nyumbani baada ya kufanyiwa matendo ya kikatili na kukiukwa kwa mikataba yao na waajiri wao, anaandika Regina Mkonde.
Hayo yamesemwa na Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.“Miezi ya hivi karibuni hususan kati ya mwezi Machi hadi Mei, 2016 balozi zetu nchini India na Malaysia zimepokea maombi ya kusaidia kuwarejesha nyumbani Watanzania ambao walipelekwa kwa ahadi za kupatiwa ajira.
“Baadhi ya wahanga wamekuwa wakikimbilia kwenye ofisi zetu za ubalozi kuomba msaada na kwamba, zilikuwa zikiwahifadhi ubalozini na kisha kuwasiliana na jamaa zao ili wawatumie nauli na kurejea nyumbani,” amesema.
Amesema, changamoto wanazokutana nazo ndizo zinawasukuma kuomba msaada wa kurejeshwa nyumbani huku akiwataka wananchi kutokubali kurubuniwa na ahadi za kwenda kufanya kazi nje ya nchi hasa zile ambazo zisizo za ujuzi.
“Wakifika huko hulazimishwa kufanya ukahaba na kunyang’anywa hati zao za kusafiria ili kudhibitiwa wasitoroke na ndiyo matatizo makubwa zaidi ambayo yamekuwa yakiwakabili watanzania,” amesema.
Sambamba na matatizo hayo, Kasiga ameeleza matatizo mengine yakiwemo ya kufanyishwakazi bila mikataba, kazi nyingi ambazo kimsingi zingetakiwa kufanywa na watu wa kada mbili au tatu pamoja kukiuka makubaliano ya awali.
Aidha, wizara imetoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano katika kutoa taarifa za watu wasio waaminifu wanaoshukiwa kujihusisha na mtandao wa biashara ya kusafiisha binadamu ambao uhusisha raia wa Tanzania waliopo ndani na nje ya nchi pamoja na wageni waliopo kwenye nchi hizo.
“Wizara inataka ushirikiano kutoka kwa wananchi katika kukabiliana na changamoto wanazozipata Watanzania nje ya nchi wakitafuta maslahi ya kiuchumi ambazo zinaviashiria vya biashara haramu ya binadamu,”amesema.
Amesema serikali haitowafumbia macho watu watakaobainika kujihusisha na mtandao huo na kwamba itawatia katika miko ya sheria kwa lengo la kutokomeza biashara hizo.
“Ni wazi kwamba vitendo hivyo ni uvunjwaji wa sheria na vya kinyama na kwamba vinakiuka haki za binadamu.Ifahamike kwamba usafirishaji wa binadamu ni uhalifu kwa mujibu wa makosa ya kupangwa ya Azimio la Umoja wa Mataifa Na. 55/25 la mwaka 2003,” amesema na kuongeza;
“Ambalo linazuia, kukomesha na kuadhibu usafirishaji wa binadamu hasa kwa wanawake na watoto chini ya itifaki yake, pia ni kinyume cha sheria ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu ya mwaka 2008.”
Post a Comment