Hali si shwari ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na mchakato unaoendelea wa kumkabidhi Rais Dk. John Magufuli uenyekiti wa chama hicho, kukumbwa na sintofahamu.
Taarifa kutoka ndani kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC), kilichofanyika juzi Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, zimethibitisha kutokea mgawanyiko wa vigogo ndani ya chama hicho.
Hali hiyo imekuja baada ya kutokea kwa mvutano juu ya tarehe rasmi ya kufanyika kwa mkutano mkuu maalumu uliopangwa Juni mwaka huu, ambao pamoja na mambo mengine Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete atakabidhi kijiti kwa Rais Magufuli.
Chanzo cha kuaminika ndani ya kikao hicho kilidokeza kuwa, kabla kilifanyika kikao kidogo kilichokuwa na wajumbe wanne ambao pamoja na mambo mengine walijadili ajenda muhimu ikiwamo ya kupanga tarehe kwa ajili ya mkutano huo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kikao hicho kidogo kilishirikisha viongozi wanne akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Jakaya Kikwete, Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Habari hizo zinaeleza kuwa, katika kikao hicho kidogo viongozi hao walikubaliana wakatangaze tarehe rasmi, na Rais Magufuli alikubali kukabidhiwa uenyekiti wa chama kama ulivyo utaratibu wa CCM lakini baada ya kikao cha Kamati Kuu kuanza, Kikwete alikataa kuruhusu hoja hiyo ijadiliwe, hatua iliyozua mfarakano.
“Baada ya kumalizika kwa kikao kile viongozi hao wanne waliingia ndani ya kikao cha CC ambacho kilikuwa na ajenda kadhaa ikiwemo ya mkutano mkuu maalumu ambapo mwenyekiti alirusha na kutaka hoja ya tarehe isijadiliwe,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, ilipofika ajenda ya tatu ambayo iliwasilishwa na Katibu Mkuu, Kinana kuhusu kutangazwa kwa tarehe ya mkutano mkuu maalumu, Kikwete aligoma isijadiliwe na badala yake aliahirisha kikao na kutoka nje.
Chanzo hicho kilisema, uamuzi wa Mwenyekiti Kikwete wa kuahirisha kikao ulijikita katika suala la gharama za mkutano ambazo zinakadiriwa kuwa ni zaidi ya Sh bilioni mbili, hivyo aliwataka wajumbe waahirishe kikao ili kutoa fursa ya kutafuta fedha.
Taarifa hizo zilieleza kuwa, kutokana na hali hiyo yaliibuka makundi mawili, moja linalomuunga mkono Kikwete na jingine linalopingana na hoja hiyo, likidai kuwa fedha si tatizo kwa chama hicho kwa kwani kina miradi, ruzuku na marafiki wengi.
“Wanaompinga mwenyekiti walishangazwa na hoja hiyo wakisema kuwa, suala la fedha ni la watendaji wa chama na si la mwenyekiti, kitendo ambacho wamekitafsiri kwamba mwenyekiti hana dhamira ya dhati ya kukabidhi chama kwa sasa,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliendelea kutoa taarifa kuwa, baada ya Kikwete kugoma kujadili tarehe alisimama mjumbe Jenista Mhagama, ambaye alipinga uamuzi huo, huku akisema suala hilo ni lazima lijadiliwe kwa kina na tarehe ya mkutano mkuu itangazwe.
“Kauli ya mwenyekiti inaonekana iliwaudhi baadhi ya wajumbe, lakini Jenista alizungumza vizuri sana na kumhoji mwenyekiti inakuaje hataki kusema lini utafanyika mkutano mkuu maalumu ili akabidhi chama.
“Maana suala la makabidhiano ni la utamaduni wa ndani ya CCM, Jenista alisema aliyekaa muda mrefu alikuwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere pekee lakini na yeye alikabidhi kwa mzee Mwinyi (Ali Hassan) na pia ilipofika wakati kama huu mzee Mwinyi naye alikabidhi kwa mzee Mkapa.
“Si hilo tu hata mzee Mkapa naye alikabidhi chama kwake (Jakaya Kikwete), sasa inakuwaje yeye leo hataki kufuata utaratibu huo ambao ni wa kawaida ndani ya chama?,” kilihoji chanzo hicho.
Chanzo kingine cha habari kilisema kuwabaada ya mwenyekiti huyo wa CCM taifa kuahirisha kikao hicho juzi, aliondoka na kurejea jijini Dar es Salaam kwa gari tofauti na ratiba iliyokuwa imepangwa.
“Ratiba ya chama ilikuwa baada ya kikao cha jana (juzi) mwenyekiti angelala Dodoma na badala yake alipoahirisha kikao kwa utata alipanda kwenye gari na kuondoa hali ya kuwa alitakiwa kurejea Dar leo (jana).
“Baada ya kikao hicho alitoka mzee Kinana akiwa amekasirika sana, tena huku akiwa amekunja sura, unajua siku zote mzee Kinana anaamini kwamba kile kilichokuwa kinapiganiwa na chama hivi sasa ndicho kinachotekelezwa na Rais Magufuli tena kwa vitendo tofauti na huko nyuma,”kilisema chanzo chetu.
Baraza la Wazee kukutana
Taarifa nyingine zinaarifu kwamba, kutokana na hali hiyo Baraza la Wazee la CCM linaloundwa na viongozi wastaafu, linatarajiwa kukutana kati ya leo na kesho kwa lengo la kujadili hali hiyo ili kuondoa mtanziko huo uliojitokeza.
“Ninachotaka kukuambia katika kipindi cha siku mbili baraza la ushauri la wazee litakutana na kujadili hali hii na baada ya hapo watakwenda kwa mwenyekiti kumshauri juu ya uamuzi wake na autafakari kwa kina.
“Tunajua tunakwenda vizuri katika hili na hakuna kitakachoharibika na wazee wetu watamshauri vema mwenyekiti ili kupata mwafaka wa kudumu na mkutano mkuu utafanyika mwezi uliopangwa,” chanzo hicho kilisema.
Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM, linaongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi (Mwenyekiti), Pius Msekwa (Katibu) na wajumbe ni Rais mstaafu Benjamin Mkapa pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu (Bara), John Malecela.
Post a Comment