Loading...

Wahariri MAWIO wang’ang’aniwa

 Simon Mkina, Mhariri wa gazeti la MAWIO (kushoto) akiagana na Afande Mhagama ambaye ni mpelelezi wa kesi hiyo
LICHA ya Serikali ya Rais John Magufuli kufuta kwenye orodha ya usajili Gazeti la MAWIO, bado ‘inakomaa’ na wahariri wake, anaandika Mwandishi Wetu.
Taarifa za ndani kutoka Jeshi la Polisi zinaeleza kuwa, Mhariri wa gazeti la MAWIO, Simon Mkina na Mhariri wa gazeti la MwanaHALISI ambaye pia alikuwa mwandishi mwandamizi wa gazeti hilo, Jabir Idrissa sasa watafikishwa mahakamani.
Mwingine anayetarajiwa kufikishwa mahakamani leo kwenye kesi hiyo ni Tundu Lissu, Mwanasheria wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa madai ya kutoa kauli za uchochezi zilizoandikwa kwenye gazeti hilo.
“Hapa nipo barabarani ninakwenda polisi kuitikiwa wito,” Mkina ameuambia mtandao huu asubuhi ya leo.
Gazeti la MAWIO lilifutwa Januari mwaka huu baada ya kudaiwa kuandika habari za uchochezi zilizohusu mgogogo wa kisiasa visiwani Zanzibar kwenye toleo lake la 182 la Januari 14-20, 2016.
Serikali kupitia Nape Nauye, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo alitangaza kulifuta gazeti hilo lililokuwa likichapishwa na Kampuni ya Victoria Media Services Ltd.
Katika tangazo lake lililotolewa kupitia gazeti la Serikali notisi namba 55 ya Januari 15, 2016 Serikali imebainisha kuwa imechukua uamuzi huo wa kulifungia gazeti la MAWIO kwa muda wote kwa mujibu wa mamlaka iliyonayo kupitia sheria ya magazeti ya mwaka 1976 sura ya 229 kifungu cha 25(1).
“MAWIO linatakiwa kusimamisha uchapishaji wake kwa kipindi chote ikiwemo pia katika vyombo vya mawasiliano vya kielektroniki kuanzia Januari 15, 2016”, ilisema sehemu ya tangazo hilo ambalo limetolewa katika gazeti la serikali, likisainiwa na waziri Nape Nauye.
Serikali ilianza kulikabili rasmi gazeti la MAWIO 31 Desemba, 2015 kwa barua iliyoandikwa na msajili wa magazeti ikimtaka mhariri wa gazeti hilo kutoa maelezo ya kwanini gazeti hilo lisifungiwe kufuatia makala zake mbili zenye vichwa vya habari “Hosea kortini” na “Seif Rais Zanzibar” ambazo zilidaiwa kuzua taharuki.
“Nakujulisha kwamba ofisi ya msajili wa magazeti haijaridhika na utetezi wako kwa kuwa hujatoa uthibitisho usio na shaka juu ya madai ya makala ulizochapisha,” ilitamka sehemu ya barua iliyosainiwa na Raphael Hokororo, kwa niaba ya msajili.
Gazeti la MAWIO lililokuwa ikiandika habari za kiuchunguzi lilikuwa likifichua kashfa mbalimbali za ufisadi, uvunjifu wa haki za binadamu na rushwa ambapo lilifuata mkondo uleule ambao gazeti la MwanaHALISI liliufuata 30 Julai 2012 pale lilipofungiwa kwa muda usiojulikana kwa madai ya kuchapisha taarifa za uchochezi.
MwanaHALISI lilikaa kifungoni kwa zaidi ya miaka mitatu kabla ya kurejeshwa kwa amri ya Mahakama Kuu mwezi Agosti, 2015 kufuatia Saed Kubenea, Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers kufungua kesi, akipinga kufungiwa kwa gazeti hilo.
Mpango wa kulifungia gazeti hilo ulitajwa kubainika mapema kufuatia kurejeshwa kwa gazeti la MwanaHALISI mnamo mwezi Agosti, 2015 na hivyo serikali kupitia msajili wa magazeti kutokuwa tayari kuvumilia machapisho ya habari na makala za kiuchunguzi kila wiki kutoka katika magazeti hayo na hivyo kutafuta namna ya kulifungia mojawapo.
Kwenye kesi ya MAWIO, Jeshi la Polisi lilimuunganisha Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Magharibi kwa madai ya kutoa hoja za uchochezi katika gazeti hilo.
Lissu alihojiwa kwa zaidi ya saa moja Makao Makuu ya Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam baada ya kuhitajika kutoa maelezo kwa madai ya kutoa kauli za uchoelezwa zilizoandikwa kwenye Gazeti la MAWIO zilizohusu mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top