Kamishna mkuu wa shirika linalosimamia maswala ya wakimbizi la Umoja wa mataifa UNHCR bwana Filippo Grandi yuko nchini Kenya kwa mazungumzo kuhusu mpango wa serikali ya nchi hiyo ya kufunga kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani ya Daadab, iliyoko kaskazini mwa Kenya ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Daadab yenye takriban wakimbizi 600,000 ni miongoni mwa kambi za wakimbizi ambazo zina idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani.
Kambi hiyo ilizinduliwa yapata miaka ishirini na tano iliyopita ilikuwapa uhifadhi raia wa Somalia ambao walikuwa wakitoroka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Hata hivyo, hivi karibuni, serikali ya Kenya imesema wakati umefika kwa kambi hiyo kufungwa.
Kenya inalalamikia utovu wa usalama kufuatia habari za kijasusi zilizodai kuwa wanamgambo wa Al Shabaab wanatumia kambi hiyo ya wakimbizi kubwa zaidi nchini Kenya kupanga mashambulizi ya kigaidi nchini Kenya.
Awali mpango sawa na huu wa kuwarejesha kwao wakimbizi haukufaulu huku serikali ya Kenya ikilaumu washirika wake yaani Serikali ya Somalia naShirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia maswala ya wakimbizi,UNHCR kwa utepetevu.
Wale wanaopinga kurejeshwa Somalia ni wale waliozaliwa katika kambi hiyo.
Ziara yake bwana Grandi inawadia siku moja tu tangu rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamoud kukamilisha ziara ya siku mbili ambayo ilimpeleka katika kambi hiyo ya wakimbizi ya Daadab ambayo iko Kaskazini Mashariki mwa Kenya mbali na kufanya majadiliano ya ana kwa ana na rais wa kenya Uhuru Kenyatta.
Post a Comment