Hatua ya Norway kutaka kumrudisha Tanzania kwa nguvu Abdulrahman anayefahamika pia kama Mustafa Mohamed Yusuph ambaye ameishi nchini humo kwa miaka 20 imeibua sintofahamu kuhusu uhalali wa mhamiaji huyo.
Wakili Erlend Anderson wa Norway, ameiandikia Serikali ya Tanzania akiitaka kuweka wazi msimamo wake, endapo imekubali kumpokea raia huyo.
Katika barua yake, wakili huyo anasema mteja wake anaishi kwa hofu na ameathirika kisaikolojia baada ya mamlaka nchini Norway kutaka kumrejesha Tanzania wakati yeye si raia wa Tanzania.
“Tangu Polisi wa hapa Norway wamjulishe kuwa ajiandae wamrudishe Tanzania tupo gizani na tunajiuliza Tanzania itampokeaje wakati ilishamkataa mwaka 2009?” alihoji.
“Mpaka Polisi wamwarifu mteja wangu kuwa wanataka kumrejesha Tanzania ni lazima wawe wamewasiliana na mamlaka za Tanzania. Tunahitaji kupata msimamo wa Tanzania,” alisisitiza.
Wakili huyo alisema endapo Tanzania itakubali kumpokea wakati ikijua si raia wake bali Somalia, watalazimika kupeleka suala hilo kwenye vyombo vya kimataifa vya haki za binadamu.
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Norway, Jacob Msekwa, alikaririwa na gazeti hili mwezi uliopita akikiri kufahamu jambo hilo lakini akataka waulizwe maofisa wa Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania.
“Hilo jambo ni very complicated (ni gumu) maana kuna madai ya mistaken identity (kumfananisha) lakini ni vizuri ukawasiliana na Migration (Uhamiaji) hapo Dar es Salaam wanalifahamu,” alisema.
Hata hivyo, Msemaji wa Uhamiaji, Abbas Irovya aliwatupia mpira Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa ndio wanaopaswa kuzungumzia suala linalohusu nchi na nchi.
“Sisi mipaka yetu inaanzia pale huyo mtu kama angekuwa ameshakanyaga ardhi ya Tanzania, lakini kwa vile bado yuko Norway, msemaji wake ni Wizara ya Mambo ya Nje,” alisisitiza Irovya.
Jitihada za wiki mbili sasa za kumpata Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika wa Wizara hiyo, Balozi Joseph Sokoine hazikuzaa matunda kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa.
Hata gazeti hili lilipomtumia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yake ya mkononi na ujumbe huo kupokelewa, mkurugenzi huyo hakujibu chochote.
Endapo mamlaka za usalama za Norway zitamrejesha kwa nguvu Abdulrahman nchini, hiyo itakuwa mara ya pili, kwani Oktoba 22,2009 alirejeshwa kwa nguvu chini ya ulinzi wa Polisi wa Norway.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu kutoka Norway, wakili wa mkimbizi huyo, Anderson, alisema Serikali ya Norway imeukataa ukimbizi wake na anaweza kurejeshwa Tanzania wakati wowote.
“Sababu ni kwamba hawaamini kuwa anatokea Somalia na wakati wowote kuanzia sasa watamkamata kumrejesha kwa nguvu Tanzania,” alisema.
Wakili huyo alisema mwaka 2009, raia huyo aliporejeshwa, mamlaka za Tanzania zilimkataa kuwa si raia wake, hivyo akarejeshwa tena Norway na kuomba upya hifadhi nchini humo.
“Maombi yake tangu kipindi hicho ndio yamekataliwa, kwa hiyo ubalozi wa Stockholm (wa Tanzania), umetoa pasi ya kusafiria ili arejeshwe tena Tanzania. Hatuelewi nini kinaendelea,” alilalamika.
Taarifa zaidi zinadai wakati Polisi Norway wakidai ni raia wa Tanzania, Abdulrahman anadai umri wake ni miaka 38 lakini anafananishwa na Mtanzania mwenye umri wa miaka 68.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Novemba 9,2009, Idara ya Uhamiaji nchini ilimwandikia Balozi wa Norway nchini, ikimtaarifu kuwa uchunguzi umethibitisha Yusuph si Mtanzania.
“Hisia za Serikali ya Norway ni kuwa Yusuph ni Mtanzania lakini baada ya uchunguzi wa kina tumebaini si raia wa Tanzania,” inasomeka barua hiyo yenye kumb IMM/HQTS/IR/65/09/53.
Katika barua hiyo iliyotiwa saini na Kamishina mkuu wa Huduma za Uhamiaji, K.W.D Kihomano, Yusuph anadai ni Msomali na ameishi Norway kwa miaka 15 hadi anarejeshwa Tanzania.
“Anadai (Yusuph) Polisi Norway walijielekeza vibaya kumrejesha Tanzania kwa nguvu na kwamba kama ni urejeshwaji basi alipaswa kurejeshwa Somalia, nchi aliyoikimbia kwa hofu,” imedai barua hiyo.
“Ni kwa maoni yetu kuwa Bwana Abdulrahman alirejeshwa kimakosa Tanzania hivyo tunalirejesha suala hili kwako ili uwezeshe kurejeshwa Norway ambako alikuwa akiishi,” alisisitiza Kihomano.
Pamoja na mwaka 2009 Tanzania kujiridhisha kuwa Mkimbizi huyo si raia wa Tanzania, bado mamlaka za uchunguzi za Norway ziliendelea kuwasiliana na mamlaka za Tanzania zikitaka zimpokee mkimbizi huyo.
Post a Comment