PAUL Nkhungwe, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Teya, Kata ya Ilindi wilayani Bahi, Dodoma amedai kuwepo kwa ufisadi wa zaidi ya Sh. 3 milioni zilizotakiwa kutumika kwenye ujenzi wa Shule ya Msingi Tegemezi Teya, anaandika Dany Tibason.
Amesema hayo katika mkutano wa hadhara ulifanyika leo kwenye shule hiyo ambapo wananchi walikuwa wakihoji fedha za ujenzi huo namna zilivyotumika na hatua gani zinachukuliwa.Katika mkutano huo ambao ulikuwa ufanywe na Omari Badwel, Mbunge wa Bahi (CCM) ambaye hakuwepo, ulifanywa na Rashid Hamsini, Diwani wa Kata ya Ilindi (CCM), wananchi wa kitongoji hicho walimtaka diwani aelezee mahali fedha zilipopelekwa.
Akizungumza katika mkutano huo Nkuhungwe ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Teya amesema, kwa sasa kuna mvutano mkubwa kati ya serikali na wananchi wa Kitongoji cha Teya kutokana na kutokuwepo kwa maelewano hususan katika kujua hatima ya shule hiyo.
Nkhungwe amesema, zaidi ya miaka 9 sasa shule hiyo iliyojengwa tangu mwaka 2007, ina darasa la awali hadi darasa la tatu na ina wananfunzi 263 lakini ina mwalimu mmoja tu.
Kiongozi huyo amesema, kutokana na kuwepo kwa uhitaji wa shule ya msingi, serikali iliwataka wananchi kutumia nguvu zao kujenga huku wakiambiwa mbunge pamoja na serikali watasaidia.
“Ikumbukwe kuwa, hapa Teya hatukuwa na shule, hii iliyopo iko Ilindi ambako ni zaidi ya kilometa 13 kutoka hapa na serikali ilisema tutakapoanza kujenga, watatusaidia baadhi ya vifaa na kuifanya shule yetu isajiliwe.
“Lakini cha kushangaza shule tumejenga licha ya serikali kusema itatusaidi sana, imesaidia baadhi ya vitu licha ya kuwa havina kiwango na halmashauri ilitoa kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 8.
“Fedha iliyotumika ni kama milioni nne hivi na ikumbukwe ilitolewa milioni 3 kwa ajili ya ununuzi wa milango na madirisha lakini fedha hizo hazionekani.
“Ilinunuliwa rangi kwa ajili ya majengo, rangi hiyo haionekani. Sasa tunataka majibu, hizo pesa ziko wapi na Shule ya Msingi Teya itasajiliwa lini,” amehoji Nkhungwe.
Katika hatua nyingine kiongozi wa Sungusungu katika kitongoji hicho Lukas Hoya amesema, kwa sasa wanafunzi ambao wanamaliza Darasa la Tatu katika shule hiyo hawaendelei na masomo kutokana na shule mama ya Ilindi kuwa mbali zaidi ya kilometa 13.
Anathor Nyakwake,Mwenyekiti wa Kata ya Ilindi amesema, suala la fedha kutafunwa limekuwa sugu kwani hata wanapo jaribu kuhoji, hawapati majibu ya uhakika.
Rashid Hamsini, Diwani wa Ilindi amesema, taarifa za kutafunwa kwa zaidi ya milioni 3 ambazo zilitakiwa kujenga shule hiyo anazo na tayari amezifikisha kwa mbunge wa jimbo hilo.
Rachel Chuwa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bahi alipoulizwa kuwepo kwa upotevu wa kiasi hicho cha pesa amesema, hajui na ni mgeni katika wilaya hiyo.
“Mimi ni mgeni katika halmashauri na tangu nimefika sijawahi kutoa fedha katika Shule ya Msingi ya Tegemezi Teya lakini nitajaribu kuangalia jambo hilo na nitakupatia majibu,” amesema Chuwa.
Post a Comment