Loading...

BREAKING NEWS: RAIS MAGUFULI AMUIBUA TENA "PROFESA YUNUS MGAYA " ALIYETUMBULIWA TCU NA KUMFUTA MACHOZI KWA KAZI NYINGINE

 KWA mara ya kwanza tangu aingie madarakani miezi saba iliyopita, Rais John Magufuli, jana alitangaza kumfuta machozi mtendaji ambaye 'alimtumbua' kwa kushindwa kutimiza matarajio
 
Alipotangaza kwamba aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Yunus Mgaya, atampa kazi nyingine.
Profesa Mgaya ni miongoni mwa Watendaji wanne wa TCU waliosimamishwa kazi na Rais kwa pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako wiki iliyopita.
Walisimamishwa kwa kosa la kudahili wanafunzi 489 ambao walifeli kidato cha nne na kukosa sifa hata za kuendelea na cheti (astashahada), kusoma vyuo vikuu shahada ya kwanza ya ualimu wa sayansi.
Mbali na kutokuwa na sifa ya kujiunga na elimu ya juu, wanafunzi hao walipewa mkopo wengi ikiwa ni asilimia 100, na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. milioni 700.
Kusamehewa kwa Mgaya kunakuja siku tano baada ya Profesa huyo na Ndalichako kuwaeleza waandishi wa habari kuwa Rais Magufuli, amemwagiza kuwasimamisha kazi watendaji waliohusika na udanganyifu.
Profesa huyo alikwenda kukabidhi ofisi TCU ambako aliwaeleza waandishi kuwa amekubali kutumbuliwa kwake.
“Nikiwa miongoni mwa watendaji waliopumzishwa kazi, nimekuja kueleza dhamira yangu ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa nchini,” alisema Profesa Mgaya na kueleza zaidi:
“Aidha ninaunga mkono jitihada za Rais Magufuli katika kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata elimu msingi bure, na elimu inayotolewa nchini inakidhi viwango stahiki kitaifa na kimataifa.”
Akizungumza na wanajumuiya, wanafunzi na wadau wa elimu kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana, Rais alisema “kwa namna ya pekee, ingawa siyo kwa umuhimu sana nataka nimsifu sana Profesa Mgaya. Ni mtanzania wa kweli.
"Walitaka kumuingizia maneno ya ovyo ovyo akasimama hadharani kwa sababu naye haungi mkono kusomesha vihiyo.
“Profesa Mgaya umetolewa kwenye uenyekiti (ukatibu)wa TCU, nitakupa uenyekiti mwingine, mimi si ndiyo rais?” Alisema na kuwaacha watu waliohudhuria wakicheka na kushangilia.
Alisema Profesa Mgaya ameonyesha uzalendo wa kweli “na ndiyo maana nazungumza kwa dhati wala siogopi kusema, mtu ukikosea kutubu ni vizuri na saa zingine unaweza kukosea kwa sababu hukuwa na njia.
"Kwa hiyo (Profesa) umeonyesha uzalendo wa kweli, utanzania wa kweli wa kuwajibu waliokuwa wanataka kupotosha, endelea hivyo na Mungu atakusaidia.”
Akiwa kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na hata baada ya kuapishwa kuwa Rais wa tano Novemba 5, mwaka jana pia, Dk. Magufuli amekuwa akiahidi kutohamisha mtendaji ambaye atakuwa ameharibu mahala pamoja, kwa nia ya kumpeleka sehemu nyingine.
Wengine waliosimamishwa kwa kushindwa kudhibiti ubora katika udahili ni Mkurugenzi wa ithibati na uthibiti ubora, Dk. Savinus Maronga, Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Rose Kiishweko na Ofisa Msimamizi Mkuu wa taarifa, Kimboka Stambuli wote wa TCU.

CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top