JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linafanya uchunguzi wa kina ili kuthibitisha taarifa za ubakaji kwa baadhi ya wanajeshi wake nchini Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo (DRC), anaandika Regina Mkonde.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuibuka kwa tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na wanajeshi wake nchini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari Meja James Macheta, Ofisa Habari wa JWTZ kwenye Makao Makuu ya Jeshi yaliyopo Upanga jijini Dar es Salaam leo amesema, jeshi haliwezi kupuuzia taarifa hizo.
“Jeshi limeanza kuchukua hatua za kiuchunguzi ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo ingawa rekodi za majukumu ya ulinzi wa amani zilizokwishafanywa na JWTZ sehemu mbalimbali, zinaonesha hakukuwa na tuhuma kama hizo,” amesema Meja Macheta.
Amesema, JWTZ bado liko imara na linaendelea kutekeleza majukumu yake nchini DRC kwa kufuata sheria na taratibu za Umoja wa Mataifa.
“JWTZ chini ya Jeshi la Umoja wa Mataifa (MUNUSCO) limekuwa likitekeleza majukumu ya ulinzi wa amani nchini Kongo takribani miaka mitatu bila ya kupata tuhuma kama hizo, tunasikitishwa na taarifa hizo,” amesema.
Amesema, jeshi katika utekelezaji wa majukumu yake lilitekeleza kwa nidhamu na weledi wa hali ya juu na kusababisha kuwa moja ya majeshi yanayofanya vizuri na kutoa mchango mkubwa katika ulinzi wa amani kwenye nchi zilizokuwa na vita.
Post a Comment