Loading...

Mgombea wa ubunge CUF adaiwa kudhalilishwa.

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, imeanza kusikiliza rasmi kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo la Pangani, kwa mashahidi wa mlalamikaji kutoa ushahidi wao.
 
Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CUF, Amina Mwindau, anayepinga ushindi wa Jumaa Awesso, inasikilizwa na  Jaji Patricia Fikirini, ambaye alisema jana kwamba atasikiliza mfululizo.
 
Katika shauri hilo, Amina anatetewa na Wakili Mashaka Ngole wakati Awesso anatetewa na Kanyama Anthony na Warehema Singano. Jopo la mawakili wa serikali wanaomtetea Mwanasheria Mkuu wa Serikali msimamizi wa uchaguzi, linaongozwa na Martenus Marandu na Saraji Iboru.
 
Akitoa ushahidi huku akihojiwa na mawakili wa pande zote, Katibu wa CUF Wilaya ya Pangani, Ramadhan Hamad, alidai kuwa  alipelekewa taarifa ofisini kwake kwamba katika mikutano ya kampeni ya CCM iliyofanyika Madanga, Mkaramo, Mwera na Mikinguni,  waliopanda majukwaani walisikika wakitoa maeneo ya kumdhalilisha na ya ubaguzi dhidi ya Amina Mwindau.
 
Alidai kuwa viongozi wa CCM waliopanda kwenye majukwaa walisikika wakisema: “Amina Mwindau katiwa mimba na Anko Moo, Amina kwao ni Mwarongo si Pangani, Amina ni mwanamke hawezi kuongoza na uchaguzi ukimalizika atakwenda Zambia kumfuata mumewe.”
 
Shahidi mwingine, Swaib Mwanyika (24) anayeishi kata ya Madanga, aliwataja viongozi aliowaona wakipanda jukwaani Madanga kuwa ni Salim Bahorera na Hamis Mnegero ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Pangani kwamba walisikika wakisema ''Amina kwao Mwarongo…Amina ni Bi Kidude.''
 
Shahidi huyo alitoa maeneo hayo kwa kuongozwa na wakili wa Mwindau, Mashaka Ngole lakini Jaji alilazimika kuahirisha kesi hiyo baada ya kumhoji wakili wa Awesso, Kanyama ambaye alidai  ana maswali 52 ya kumhoji Mwanyika na kutokana na kuwa zilibaki dakika 41 kutimia saa 10.00 jioni, hawezi kufanya hivyo.
 
Idadi ya mashahidi waliopangwa kutoa ushahidi wao katika shauri hilo ni  94. Mashahidi wa Mwindau ni 48 na waliobaki ni wa upande wa Awesso.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top