Loading...

Hali inatisha bungeni

 Wabunge wa Ukawa wakizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge huku wakiwa wameziba plasta midomoni
KAMA mdhaha vile. Moto unazidi kufukuta kati ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wanaotoka vyama vya upinzani bungeni, anaandika Faki Sosi.
Mpasuko katika makundi hayo mawili (chama tawala na upinzani) unatishia usalama wa umoja unaohitajika katika kusimamia serikali kwa mujibu wa chombo hicho.
Taarifa zilizofikia mtandao huu zinaonesha kwamba, tayari uhasama kati ya CCM na upinzani umefika pabaya na hata kutengana katika baadhi ya mambo ambayo walikuwa wakifanya kwa pamoja nje ya Bunge.
Pia kauli za matusi, kejeli na dharau zinaendelea kushamiri jambo ambalo limezidisha mpasuko huo. Hatua hiyo imeongeza kuyumba kwa Bunge.
Msingi wa kukithiri myumbo huo ni kutokana na hatua ya upinzani kususa kushiriki vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge.
Hatua ya wabunge wa upinzani jana kutoka bungeni huku wakiwa wamefunga midomo yao kwa plasta imekwenda sambamba na kujiondoa kwenye mitandao ya kijamii inayounganisha ikiwa ni pamoja na ule wa Whatsapp.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, hatua hiyo ya kujiondoa kwenye mitandao ya kijamii inatokana na wabunge wa CCM kudaiwa kuwa wanachangia kumpa jeuri Dk. Tulia kuendesha Bunge kwa ubabe pia kuwaminya wapinzani.
Hatua hiyo ya wabunge hao kujiondoa kwenye mitandao ya kijamii ilitanguliwa na ile ya wabunge wanawake kutoka upinzani kujiondoa kwenye umoja wa wanawake wa wabunge wote (wanawake) baada ya upinzani kutukanwa na mbunge wa CCM kwamba, ndani ya upinzani mwanamke hapewi nafasi mpaka aitwe baby’ kwa maana ya kutoa penzi.
Jana wakati wabunge wa upinzani wakitoka nje ya Bunge na kumsusia Dk. Tulia kuendesha kikao hicho, walikuwa wakizomewa na wabunge wa CCM.
Hatua ya upinzani kutoka nje ni mwendelezo wa kugomea vikao vinavyoongozwa na Dk. Tulia ambaye anatuhumiwa kuminya uhuru wa wabunge wa upinzania na kupendelea wabunge wa CCM.
Wabunge hao wa upinzani baada ya kutoka nje, walikwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya African Dream na kufanya kikao chao cha faragha.
Hata hivyo, hatua ya kuziba midomo kwa plasta imeelezwa kwamba, ni kuonesha wazi kuwa Bunge linawafunga midomo wapinzani na kuminya demokarasia.
Staili ya jana ni tofauti na ile ya awali ambapo wabunge walikuwa wakitoka bungeni kimya kimya, safari hii wametoa ujumbe mpya kwa Dk. Tulia.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top