Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), George Simbachawene, amemwuomba Rais John Magufuli kufanya
uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya, baada ya Juni 30, mwaka huu, siku
ambayo wanatakiwa wawe wametatua tatizo la madawati.
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akifungua mkutano wa Umoja wa Maofisa
Elimu wa Mikoa na Wilaya nchini (REDEOA), uliofanyika mjini hapa.
Simbachawene alisema ni vyema utatuzi wa madawati katika maeneo yao utumike kama kigezo cha uteuzi wao.
"Ningependa nimwombe Rais asubiri hadi Juni 30 ipite, maana tulishaagiza
hadi tarehe hiyo kuwe hakuna mwanafunzi anayekaa chini na hicho
kitakuwa kipimo kimojawapo," alisema Simbachawene.
Alisisitiza kuwa wakuu wa mikoa na wilaya watakaoshindwa kutimiza suala
hilo, hali zao zitakuwa mbaya na watakuwa hawatoshi kuendelea katika
nafasi zao.
Alizitaka halmashauri kuhakikisha madawati ya wanafunzi yanapatikana kwa wanafunzi wote.
Kuhusu wanafunzi waliozuiwa matokeo yao na vyeti, Simbachawene alisema
atakaa na mawaziri wenzake, wakiwamo wenye wanaoshyughulika na elimu na
pamoja na fedha, kumwomba Waziri Mkuu kuangalia uwezekano wa kuwasamehe
wanafunzi hao fedha wanazodaiwa ili waweze kupata vyeti na matokeo yao.
"Mimi nadhani kama tumeshaaanza mpango wa elimu bure, sioni umuhimu wa
vyeti kuzuiwa au kufungiwa matokeo wanafunzi. Tuwape tu maana hata
tukizuia wazazi bado hawana uwezo wa kulipa," alisema.
Alisema hadi sasa, zaidi ya Sh. bilioni 6.1 zimetumwa Baraza la Taifa la
Mtihani (Necta) kwa ajili ya maandalizi ya mitihani ya taifa.
Akizungumzia tatizo la usafiri kwa maofisa elimu mikoa na wilaya,
Simbachawene aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala wa
mikoa kuhakikisha wanatenga magari kwa ajili ya maofisa hao.
Kuhusu ruzuku ya uendeshaji, fidia ya ada na chakula, Simbachawene
alisema mpango wa elimu bure ulianza baada ya bajeti ya mwaka 2015/16
kupita, jambo ambalo limefanya uendeshwe kiugumu lakini limeleta
mafanikio.
Post a Comment