Loading...

MAWIO wapangua mashtaka mawili

Simon Mkina, Mhariri wa gazeti la MAWIO (katikati) akizungumza na waandishi wa habariMAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam leo imewafutia mashitaka mawili Siomon Mkina, Mhariri wa Mawio na Jabir Idrisa, mwandishi wa gazeti hilo na Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, anaandika  Faki Sosi.
Ni katika kesi ya uchochezi iliyofunguliwa na serikali dhidi ya watu hao pamoja na mchapishaji wa gazeti la Mawio, Ismail Mahboob wa Kampuni ya Flint Graphics.
Mashitaka yaliyofutwa ni shtaka namba moja na shtaka namba tano ambapo pande zote mbili (utetezi na mashtaka) zimeridhia kufutwa kwa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Thomas Simba.
Mashtaka hayo ni kupanga njama za kufanya chapisho la uchochezi na kosa la pili ni kuwatisha wananchi wa Zanzibar kwamba, machafuko yanawaweza kutokea Zanzibar.
Awali, Poul Kadushi, Wakili wa Serikali aliiomba mahakama hiyo kuondoa shtaka namba moja na tano kutokana na kukosekana kwa idhini ya Mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Peter Kibatala, Wakili wa Upande wa Washitakiwa amesema kuwa, Wakili wa Serikali amefanya busara kukubaliana na upande huo kuwa, mashtaka hayo yalikuwa na upungufu kisheria.
Hakimu Simba amefuta mashtaka hayo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kwamba, watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu pekee.
Shitaka la pili la kuchapisha chapisho la uchochezi linawakabili Idrisa mshitakiwa namba moja, Mkina ambaye ni mshitakiwa namba mbili na Lissu, mshitakiwa namba nne.
Shitaka la tatu la kuchapisha magazeti bila ya kuwa na hati ya kiapo kutoka kwa msajili wa magazeti linamuhusu Mahboob, mshitakiwa namba tatu.
Shtaka namba nne la kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar ya kutopiga kura kwa kuhofia umwagikaji wa damu.
Hata hivyo, Kadushi amejibu hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo na upende wa utetezi kuwa, zina kasoro.
Kadushi amedai kuwa  mashitaka yote yaliyobaki katika shauri hilo yameanishwa  kwa kila kosa na kifungu chake na maelezo ya kosa hilo.
Amedai kuwa, kifungu namba 32 (a), (b), na (c) cha makosa ya jinai kimeanisha kuwa, na nia ya kutenda kosa ni kosa na kutenda kosa ni kosa.
Peter Kibatala amedai kuwa, bado hoja za Kadushi hazina mashiko na kwamba, mashtaka  hayo ya matatu yaliyobaki hayana mashiko kutokana na kwamba, Sheria ya magazeti haifanyi kazi Zanzibar na kuwa chapisho hilo lingeleta athari Zanzibar na sio Tanzania Bara ambapo yupo waziri husika.
Kibatara amewasilisha hoja ya kufutwa kwa mashtaka yaliyobaki kwa madai kuwa, hayana mashiko kwa mujibu  wa kifungu 31(a)(b) na (c) cha sheria ya magazeti ambayo inampa haki raia kuikosoa serikali.
Kesi hiyo itatajwa tena 11 Julai mwaka huu ambapo hakimu atatoa maamuzi ya kufutwa ama kutofutwa kwa shauri hilo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top