Loading...

BREAKING NEWS: TUNDU LISSU KIBOKO MAHAKAMA YAFURIKA, LISSU AFUNGUKA NA MAHAKAMA YAFUTA MASHTAKA DHIDI YAO

Simon Mkina, aliyekua Mhariri Mkuu wa Gazeti la Mawio (Wakwanza),na Tundu Lissu, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani wakizungumza na wanahabari baada ya kutoka MahakamaniTUNDU Lissu, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ameseme kuwa, vitendo vinavyofanywa na serikali ya sasa ni vya hovyo, anaandika Faki Sosi.
Lissu ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema pia Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki amesema hayo leo muda mfupi baada ya kumaliza kusikiliza shauri lake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Kwenye shitaka hilo, Lissu pamoja na washitakiwa wengine watatu wanadaiwa kufanya makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchochezi kupitia gazeti la Mawio la tarehe 14 Januari 2016.
Kwenye gazeti hilo lililoandikwa kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’ Lissu alinukuliwa kama mchangiaji wa gazeti hilo ambapo tayari limefutwa na serikali.
Nje ya mahakamani hiyo Lissu amesema “nchi yetu imeingia katika giza nene, huyu dikteta uchwara, naomba nirudie tena, huyu dikteta uchwara anahitaji kupingwa na kila mwananchi.
“Kila msema kweli wa nchi hii. Huu ni wakati wa kujitokeza na kusema hii ni nchi ya vyama vingi, hii ni nchi inayotambua haki za binadamu kwenye Katiba yake.
“Hatuwezi tukakubali nchi iongozwe kwa kauli za mdomo za mtu mmoja hata kama amechaguliwa kuwa rais,”
Akizungumzia kesi iliyofunguliwa na kuhusishwa kwake Lissu amesema, kesi iliyofunguliwa na serikali dhidi yake na wahariri wa gazeti la Mawio ya uchochezi, ni ushahidi tosha kuwa nchi imeingia kwenye giza nene la udekikteta.
Amesema, hata sheria ya magazeti ya mwaka 1976  ipo wazi  kwamba, kuikosoa serikali sio uchochezi.
“Mashtaka haya yanayodaiwa kuwa ni ya uchochezo, sio ya uchichozi hata kidogo. Nilichosema, niliulizwa na waandishi … niliosema uchaguzi wa marudio ya uchaguzi Zanzibar yanaweza  kuviingiza visiwani hivyo kwenye machafuko na umwagaji damu… ni kauli ya raia anayefahamu na hapendezwi na mwenendo wa serikali” amesema Lissu.
Amesema kuwa, hata sheria ya magazeti inasema kuwa kitetendo chochote chenye lengo la kueleza ubovu wa serikali au mamlaka yake sio kosa.
“Nilichosema mimi kuwa serikali hii na matendo yaki ni ya hovyo… huyo dikitekta uchwara anahitaji kupingwa na kila mwananchi,” amesema.
“Kama wanafikiria watatutisha kwa kutuleta mahakamani, tutamkabili mahakamani na tutamkabili nje.
“Ni wakati wa wazalendo kusema kuwa, Tanzania ni nchi ya vyama vingi na ina Katiba na sheria. Katiba yetu inatambua haki za binaadamu na moja haki za binaadamu ni kueleza ujinga wa watawala wanapofanya ujinga,” amesema.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam leo imewafutia mashitaka mawili Siomon Mkina, Mhariri wa Mawio na Jabir Idrisa, mwandishi wa gazeti hilo na Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, anaandika  Faki Sosi.
Ni katika kesi ya uchochezi iliyofunguliwa na serikali dhidi ya watu hao pamoja na mchapishaji wa gazeti la Mawio, Ismail Mahboob wa Kampuni ya Flint Graphics.
Mashitaka yaliyofutwa ni shtaka namba moja na shtaka namba tano ambapo pande zote mbili (utetezi na mashtaka) zimeridhia kufutwa kwa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Thomas Simba.
Mashtaka hayo ni kupanga njama za kufanya chapisho la uchochezi na kosa la pili ni kuwatisha wananchi wa Zanzibar kwamba, machafuko yanawaweza kutokea Zanzibar.
Awali, Poul Kadushi, Wakili wa Serikali aliiomba mahakama hiyo kuondoa shtaka namba moja na tano kutokana na kukosekana kwa idhini ya Mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Peter Kibatala, Wakili wa Upande wa Washitakiwa amesema kuwa, Wakili wa Serikali amefanya busara kukubaliana na upande huo kuwa, mashtaka hayo yalikuwa na upungufu kisheria.
Hakimu Simba amefuta mashtaka hayo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kwamba, watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu pekee.
Shitaka la pili la kuchapisha chapisho la uchochezi linawakabili Idrisa mshitakiwa namba moja, Mkina ambaye ni mshitakiwa namba mbili na Lissu, mshitakiwa namba nne.
Shitaka la tatu la kuchapisha magazeti bila ya kuwa na hati ya kiapo kutoka kwa msajili wa magazeti linamuhusu Mahboob, mshitakiwa namba tatu.
Shtaka namba nne la kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar ya kutopiga kura kwa kuhofia umwagikaji wa damu.
Hata hivyo, Kadushi amejibu hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo na upende wa utetezi kuwa, zina kasoro.
Kadushi amedai kuwa  mashitaka yote yaliyobaki katika shauri hilo yameanishwa  kwa kila kosa na kifungu chake na maelezo ya kosa hilo.
Amedai kuwa, kifungu namba 32 (a), (b), na (c) cha makosa ya jinai kimeanisha kuwa, na nia ya kutenda kosa ni kosa na kutenda kosa ni kosa.
Peter Kibatala amedai kuwa, bado hoja za Kadushi hazina mashiko na kwamba, mashtaka  hayo ya matatu yaliyobaki hayana mashiko kutokana na kwamba, Sheria ya magazeti haifanyi kazi Zanzibar na kuwa chapisho hilo lingeleta athari Zanzibar na sio Tanzania Bara ambapo yupo waziri husika.
Kibatara amewasilisha hoja ya kufutwa kwa mashtaka yaliyobaki kwa madai kuwa, hayana mashiko kwa mujibu  wa kifungu 31(a)(b) na (c) cha sheria ya magazeti ambayo inampa haki raia kuikosoa serikali.
Kesi hiyo itatajwa tena 11 Julai mwaka huu ambapo hakimu atatoa maamuzi ya kufutwa ama kutofutwa kwa shauri hilo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top