''Watu walipoanza kusemasema, yule waziri alimwandikia Waziri Mkuu barua
ya kujiuzulu, lakini Waziri Mkuu kwa jinsi alivyokasirika wala
hakumjibu. Alichagua mtu wa kumridhi, wala hakumjibu.”
Hayo ni baadhi ya maneno yaliyo kwenye hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere,
aliyoitoa mwaka 1995 katika Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es
Salaam, alipozungumzia misingi ya miiko ya viongozi na Rais ambaye
anatakiwa kuiongoza nchi kwenye uchaguzi uliotarajiwa kufanyika mwaka
huo.
Mfano huo alioutoa Nyerere juu ya kumwajibisha kiongozi wa umma, unaweza
kutafsiriwa kuwa ndio uliotumiwa kutengua uteuzi wa aliyekuwa Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ambaye tangu kuanza utumishi wake wa
umma, hajawahi kutuhumiwa kwa namna yoyote ile hadharani.
Sambamba na mfano huo, kumekuwa na simulizi juu ya aliyekuwa mtawala wa
dola ya Roma, Julius Ceaser, ambaye wakati fulani alikwenda vitani na
baada ya kurejea alipata fununu kuwa mkewe alikuwa anatembea (kufanya
mapenzi) na mmoja wa majenerali wa akiba waliokuwa wamebaki nyumbani
wakati wa vita.
Kutokana na tuhuma hizo, mtawala huyo aliunda tume na kufanya uchunguzi
kisirisiri na hatimaye kubaini kuwa maneno hayo yalikuwa ya uongo.
Pamoja na taarifa za tume hiyo, Ceaser alimpa talaka mkewe huyo kwa kuwa
tuhuma zilizokuwa zimetolewa dhidi yake zilikuwa zinamwondolea sifa ya
kuwa mke wa kiongozi mkuu.
Hivi karibuni gazeti moja la kila wiki, kwa mara ya kwanza lilimtuhumu
mwanadiplomasia hiyo kuhusika na kampuni ya Kichina ya CRJE, ambayo
pamoja na mambo mengine, ilimejenga daraja la Kigamboni, ambalo
linadaiwa gharama zilizotumika kulijenga zimeongezwa maradufu
ikilinganishwa na gharama halisi.
Taarifa za gazeti hilo ambazo baadaye zilikanushwa vikali na Idara ya
Habari Maelezo, zilidai pia kwamba Balozi Sefue alihusika kutoa ushauri
mbovu wa kumpata Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Wiki moja tangu kutolewa kwa tuhuma hizo ambazo ghafla zilibadilisha
sifa ya Balozi Sefue, jambo hilo lilichukua sura mpya juzi, baada ya
Rais John Magufuli kutangaza kumteua Balozi John Kijazi, kushika wadhifa
aliokuwa nao Sefue.
Wakati hilo likitokea, Balozi Sefue alikuwa bado ofisini na siku moja
kabla alikuwa amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari juu ya uteuzi
tata wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii
(NSSF), Dk Carina Wangwe, uliodumu kwa takribani saa tano kabla ya
kutenguliwa.
Maelezo ya Rais Magufuli wakati akitangaza kutengua uteuzi wa Balozi
Sefue, bado hayamsafishi mwanadplomasia huyo na kashfa alizotuhumiwa
nazo hivi karibuni na badala yake, yanaacha maswali zaidi.
“Nipende kuanza kushukuru Watanzania wanavyotoa ushirikiano kwa shughuli
zinazofanywa na serikali yangu, lakini pia napenda kuchukua nafasi hii
kumshukuru Balozi Ombeni Sefue kwa jinsi ambavyo amekuwa akifanya kazi
zake vizuri.
“Na natambua ukweli kwamba amenisaidia sana katika kufanya kazi nzuri
katika kipindi cha miezi mitatu na siku kadhaa wakati nikiwa ofisi hii
hapa Ikulu, kwa hiyo nampongeza kwa kazi nzuri ambazo amekuwa akifanya.
Lakini kwa kutambua hilo pia, nimeamua kufanya mabadiliko kidogo.
“Nimeamua kumteua Balozi Injinia John Kijazi, Balozi wetu kule India
kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Balozi Sefue nitampangia kazi nyingine,
asante,” alisema Rais Magufuli.
Kutokana na maelezo hayo kutotoa jibu la kuondolewa kwa Balozi Sefue,
ndiko kunakotoa fursa kuamini kwamba tuhuma dhidi yake hata kama si za
kweli, ndizo zilizofanya uteuzi wake utenguliwe.
Balozi Sefue amekuwa Ikulu kama Mwandishi wa Hotuba za Rais tangu mwaka
1993, chini ya Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, na baadaye
kuendelea na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa mpaka mwaka 2005.
Baada ya hapo, Balozi Sefue aliendelea kushika nyadhifa za kidplomasia
kwenye nyanja mbalimbali mpaka Desemba 31, 2011, Rais wa awamu ye nne,
Jakaya Kikwete, alipomteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, kuchukua nafasi ya
Philemon Luhanjo.
Baada ya Rais Magufuli kuapishwa Novemba 5, mwaka jana, aliendela
kufanya kazi na Balozi Sefue na Desemba 30, mwaka jana, aliteua
makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wapya na kuthibitisha kwamba
ataendelea na Balozi Sefue kwenye nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi.
Mwenyewe afunguka
Jana, Balozi Sefue alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa Balozi Kijazi
kuridhia wadhifa huo na baada ya tukio hilo, aliwaeleza waandishi wa
habari kuwa haikuwa lazima kwake kuendelea na Rais Magufuli.
“Namshukuru sana Rais Jakaya Kikwete kwa kuniteua katika nafasi hii
alinipa heshima. Pili namshukuru Rais Magufuli kwa kuwa hakuwa na lazima
ya kuendelea na mimi lakini akaona katika kipindi hiki cha mpito
nimsaidie. Najisikia nimeheshimika sana kuwa pembeni yake katika mwanzo
wa serikali ya awamu ya tano,” alisema na kuongeza:
“Nitampa mwenzangu kila aina ya ushirikiano kwa sababu awamu hii
inaashiria mabadiliko makubwa katika nchi yetu. Ni vizuri kila mtu tumpe
ushirikiano ili kuhakikisha malengo ya Rais yaweze kutimia.”
Alipoulizwa ulinganifu wa utendaji kazi wa serikali ya awamu nne na ya
tano, alijibu “Hapa Kazi Tu” na kuondoka eneo alilokuwa anahojiwa na
waandishi.
Kijazi aweka yake
Kwa upande wake, Balozi Kijazi alisema utumbuaji majipu na kubana
matumizi ni endelevu ili kuiwezesha serikali kujiendesha kwa kodi yake.
Alisema mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano umeshawekwa na Rais kuwa
yapo mambo ya kipaumbele ambayo rais ameanza kuyashughulikia kama
kuongeza ukusanyaji kodi.
“Serikali yoyote duniani inaendeshwa kwa mapato na jukumu lake kubwa ni
kuhudumia wananchi, ambao ili wahudumiwe vizuri ni lazima kodi
ikusanywe, kupiga vita rushwa ndani ya vyombo vya serikali, Wizara na
taasisi, ni kipaumbele cha rais lazima nimsaidie kuhakikisha utumishi
unakuwa ni utumishi uliotukuka, wenye tija na nidhamu,” alibainisha.
Alisema atahakikisha kunakuwa na utumishi wenye motisha ili kuwezesha watumishi watekeleze majukumu yao.
Post a Comment