Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chaso), wametishia kufanya maandamano ikiwa Chuo Kikuu Cha Dodoma
(UDOM), hakitamrejesha chuoni hapo mwanafunzi wa chuo hicho, Victor
Byemelwa, aliyemsimamishwa kwa kile wanachodai ni sababu za kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaama jana,
Mwenyekiti wa Umoja huo, Jafary Ndege, alisema wanataka chuo hicho
kimrejesha masomoni haraka na kwamba ikiwa hawatafanya, hivyo
wataandamana kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kushinikiza arudishwe.
“Tunawataka viongozi wa chuo hicho kumrejesha shuleni mwanafunzi huyo
na kama wataendelea kukaa kimya tutafanya maandamano makubwa ya
kushinikiza chuo hicho kimrudishe masomoni mwenzetu na yataanzia Dar es
Salaam kwenda Dodoma katika siku ambayo tutatoa taarifa kwenye vyombo
vya habari iwapo ombi letu litapuuzwa,” alisema mwenyekiti huyo.
Ndege aliitaka serikali kutoa onyo kwa wanasiasa na kuacha kuingilia
utendaji wa vyuo vikuu kama ilivyotokea kwa chuo hicho na kusababisha
kufukuzwa mwanafunzi huyo kupitia kwa mshauri wa wanafunzi kwa barua
yenye kumbukumu no Re.UDOM/DOS/36 ya Februari 5, 2016.
Kuhusu, suala la kufutiwa usajili kwa vyuo vishiriki vya St. Joseph
Songea na Arusha, na baadhi ya vitivo katika Chuo Kikuu cha Kampala Dar
es Salaam, alisema wameshangazwa na hatua hiyo iliyochukuliwa na Tume ya
Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuwa imechangia kwa kiwango kikubwa
kurudisha nyuma maendeleo ya wanafunzi wa vyuo hivyo.
Alisema kama TCU ilikuwa inafahamu kwamba havikuwa vimekidhi vigezo ni
vema isingevipa usajili kuliko usumbufu unaotokea kwa wanafunzi hao hivi
sasa.
Post a Comment