Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Pololet Mgema, amemwomba Naibu Waziri wa
Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwele, kuridhia kutoa Sh. milioni 300 kwa
ajili ya ujenzi wa bwawa la Mitumbati lenye uwezo wa kuhifadhi ujazo wa
mita za mraba 117,000, ambalo limepasuka.
Mgema alisema juzi kuwa kupasuka kwa bwawa hilo kumeathiri zaidi ya kaya
2,000 ambazo zinajumuhisha vijiji vya Ntila, Mwenge, Farm III, Nammanga
na Mitumbati, ambazo zinakosa maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Alisema ili kukarabati bwawa hilo na kulirejesha katika hali yake ya
kawaida, linahitaji kiasi hicho cha fedha. Pia alisema kupasuka kwas
bwawa hilo kumeharibu zaidi ya ekari 120 za mazao.
“Mazao yaliyoathirika ni mahindi, mpunga, jamii ya kunde na ya bustani.
Mazao haya yalikuwa katika vijiji hivyo na huenda kukaathiri mavuno
katika msimu huu,'' alisema.
Pia alisema ekari 50 za mradi wa umwagiliaji zimeharibiwa na maji ambayo
yalikuwa katika bwawa hilo na kwamba zaidi ya mifugo 440 itakosa maji
ya kunywa ambayo ilikuwa ikitegemea kutoka kwenye bwawa hilo.
Akisoma taarifa ya skimu ya umwagiliaji ya Mitumbati ambayo pia
imeharibiwa na maji baada ya kupasuka bwawa hilo, Mtendaji wa Kijiji
hicho, Janeth Chisunga, alisema mradi huo ulikuwa ukinufaisha kaya 80
zenye jumla ya ekari 120.
Chisunga alisema kutokana na athari hiyo, zaidi ya tani 300 za chakula
zinahitajika kwa ajili ya wakulima wa vijiji vilivyoathirika kwa
kupasuka kwa bwawa hilo muhimu.
Kwa upande wake, Naibu wa Waziri huyo alisikitishwa na athari hiyo
ambayo wananchi imewapata na kuahidi kutoa kiasi hicho cha fedha
kinachohitajika.
Kamwelwe aliutaka uongozi wa wilaya kuendelea kufanya naye mawasiliano
ili mchakato wa upatikanaji wa fedha hizo uharakakishwe. Aliahidi
kwamba akifika ofisini wiki hii ataonana na Katibu Mkuu wa Wizara ili
kumweleza suakla hilo na hatimaye kutoa fedha.
Post a Comment