Baadhi ya jamii nchini zimebuni mbinu mpya ya kuendeleza mila potofu za ukeketaji wanawake kwa kuwahamisha kutoka nyumbani kwao kuwapeleka maeneo ya mbali ili wanajamii wasitambue kinachoendelea.
Utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania
(Tamwa) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Idadi ya watu Duniani (UNFPA) katika mikoa 12 ya
Tanzania Bara na Zanzibar, umebaini kuwa ukeketaji na ndoa za utotoni
bado ni tatizo kubwa.
Mratibu wa Kitengo cha Usuluhishi Tamwa, Gladness Munuo, alisema kuanzia
Januari hadi Oktoba, 2015 katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma
asilimia 39.9 ya wanawake wajawazito walifanyiwa ukeketaji.
Alisema wilaya ya Tarime kesi 118 za ubakaji ziliripotiwa mahakamani,
Pemba wasichana wadogo 240 walipata mimba mwaka 2015, huku wilaya ya
Mkalama wanawake 2,265 ambao walijifungua katika vituo vya matibabu 115,
walifanyiwa ukeketaji.
Alisema katika Kata ya Msalala wilaya ya Kahama wasichana 605 ambao ni
sawa na asilimia 47.47 kati ya 1,150 hawakumaliza shule za sekondari kwa
sababu ya ndoa za utotoni, huku katika wilaya ya Bagamoyo wasichana 12
wa shule waliripotiwa kupata mimba ndani ya miezi sita kuanzia Januari
hadi Juni, 2015.
Munuo alibainisha kuwa katika maeneo ya Tarime, wasichana hupakwa unga
usoni ikimaanisha kuwa hawakeketwi teni, lakini ukweli ni kwamba
wamewakeketa na kufanya hivyo ni kuficha ukweli.
Alisema kwa upande wa ndoa za utotoni, umebaini kuwa ndoa nyingi chanzo
kikubwa ni wazazi na ndigu kwa lengo la kupata mahari na wameshiriki
kushawishi watoto wafeli mitihani ili iwe sababu ya wao kuolewa.
“Utafiti umebaini visababishi sugu vya ukeketaji na ndoa za utotoni ni
pamoja na mila, tamaduni na desturi potofu, umaskini uliokithiri,
kukosekana kwa uelewa juu ya haki za binadamu, mfumo dume, ukosefu wa
sera imara pamoja na sheria dhaifu ambazo utekelezaji wake hauridhishi,
ukosefu wa mabweni, wanafunzi kutembea umbali mrefu hadi shuleni na
mwamko mdogo wa wazazi juu ya umuhimu wa kuwaelimisha watoto wa kike,”
alibainisha.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment