Wakati Tanzania ikiungana na nchi zingine duniani kuadhimisha Siku ya Wanawake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) ni jipu na linatakiwa kutumbuliwa.
Kutokana na tatizo hilo, Ummy amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TWB, Margareth Chacha, kutoa maelezo ndani ya siku tatu kwa nini benki hiyo inatoza riba kubwa zaidi ya asilimia 19 kwa mikopo inayotolewa.
Waziri huyo alisema juzi akiwa kwenye shughuli ya wanawake wa mkoa wa
Dar es Salaam kupitia Vyama vya Kuweka na Kukopa (vikoba) pamoja na
Benki ya Posta, wanawake walikuwa wakilalamikia kuhusu tozo kubwa ya
riba kwenye benki ya wanawake.
“Zama hizi ni za uwazi na ukweli. Nilisikitika sana benki hii inatoa
riba zaidi ya asilimia 19. Siwezi kulikubali hili, wanawake
wanaishangilia benki nyingine badala ya benki yao. Mkurugenzi (alikuwapo
kwenye hafla hiyo) una kazi ya kufanya, siwezi kusimama kutetea benki
ya wanawake kwa hali kama hizi,” alisema na kuongeza:
“Nitahitaji maelezo ndani ya siku tatu. Hizi ni zama za Magufuli, hakuna
kuoneana aibu, kwa nini benki si rafiki kwa wanawake wakati inapewa
fedha na serikali. Hili ni jipu tutalitumbua” alisema.
Alisema wanawake walikuwa wanaishangilia Benki ya Posta ambayo riba yake ni asilimia 11 na kuilalamikia yao.
Katika hotuba yake iliyosomwa na waziri huyo, Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan, aliagiza Halmashauri zote zihakikishe zinatenga asilimia
tano ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake.
Alisema wakurugenzi ambao halmashauri zao hazitatekeleza hilo watawawajibisha.
Pia alitaka wakurugenzi watenge maeneo maalum ya biashara ikiwa ni
pamoja na na kufuta kodi zenye kero kwa wajasiriamali ambao wengi wao ni
wanawake.
Alisema ripoti ya Mapitio ya Sera ya Biashara za Kati na Ndogo ya mwaka
2013, inaonyesha wanawake wanamiliki asilimia 64 ya biashara hizo,
wakati utafiti wa hali ya uchumi wa mwaka 2010 ukionyesha asilimia 23 ya
wanawake wana kipato kisichozidi au kulingana na waume zao.
Akikazia suala la wakurugenzi, Mwalimu alisema watakaoshindwa kutenga asilimia tano majina yao yatawasilishwa Ikulu.
“Mimi na naibu wangu, Dk. (Hamis) Kigwangalah, hatutashindwa
kuwawajibisha wakurugenzi wote ambao hawatatenga asilimia tano kwa ajili
ya mfuko huu, asiyetenga huyu ni adui wa wanawake, tutampelekea jina
kwa Rais Magufuli, usawa wa jinsia utafikiwa kwa kuwaendeleza wanawake
kiuchumi na kielimu,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Tukikaa kimya hii kauli mbiu ya asilimia 50/50 hadi
ifikapo 2030 itakuwa kwa wabunge lakini vijijini haitafikiwa.”
Ummy alisema katika kufuatilia utekelezaji wa suala hilo, kila robo na
nusu ya mwaka watakuwa wakitoa orodha ya majina ya wakurugenzi wote
wanaozembea kufanya hivyo.
Alitolea mfano mkoa wa Dar es Salaam ambao unatengewa Sh. bilioni 47 ya
bajeti na kusema ile inayoenda kwenye mfuko wa wanawake ni Sh. bilioni
2.3, ambayo ikitekelezwa maisha ya wanawake yatabadilika.
“Hatuwezi kusubiri hadi tutumbuliwe. Tutaanza kuwatumbua ninyi ambao
hamtekelelezi hili na kuwanyima wanawake ambao ni asilimia 64 ya watu
wote wanaofanya biashara ndogo na za kati,” alisema.
Pia aliziagiza halmashauri zitenge maeneo maalumu ambayo wanawake watafanya biashara bila kunyanyaswa.
Kadhalika, alisema kila miezi mitatu watakuwa wakizitangaza Halmashauri
ambazo zimefanya vizuri na vibaya kwenye suala la vifo vya wajawazito.
Alisema watalivalia njuga suala hilo kwa sababu lengo la serikali ni kuvipunguza vifo hivyo.
Kuhusu ukatili, Ummy alisema vitendo hivyo vipo kwa asilimia 39 nchini ambapo kwa mkoa wa Dar es Salaam vipo kwa asilimia 31.
Alisema kwenye upande wa uandikishaji wa darasa la kwanza, wamefanikiwa
kwa asilimia 50 lakini changamoto iko sekondari kutokana na mimba za
utotoni.
Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, kwa
jitihada aliyoifanya kuhakikisha inajengwa shule ya wasichana ya bweni,
ambayo itasaidia kupunguza changamoto hiyo kwa kiasi fulani.
Kuhusu likizo za uzazi, aliwataka wanawake ambao wananyanyaswa, iwe
sekta binafsi au ya umma, kutoa taarifa kwake ili mwajiri achukuliwe
hatua za kisheria.
“Hili ni tatizo ambalo linafanya baadhi ya wasichana kuogopa kubeba
mimba kwa kuhofia kufukuzwa. Tuleteeni taarifa tutawafikisha
mahakamani,” alisema.
Ummy alisema wataungana na Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Simon Sirro, kuhakikisha wakati wa ukamataji wa ‘makahaba’,
wanaume ambao ndio wateja wao, nao wakamatwe.
Akizungumzia ahadi ya Rais Magufuli ya kutoa Sh. milioni 50 kila kijiji,
alisema watakahikisha nusu yake zinaelekezwa kuwasaidia wanawake
nchini.
Pia alisema watapambana na wanaume wanaowapa ujauzito wanafunzi na
kukamata wazazi ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao wa malezi.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angellah
Kairuki, aliwataka watumishi wa umma wanawake kujiendeleza kielemu ili
waweze kushika nyadhifa mbalimbali.
Katika maadhimisho hayo, Mbunge wa Njombe, Edward Mwalongo, amepewa tuzo
baada ya kauli yake Bungeni kuhusu wanafunzi wa kike wanavyokosa masomo
kutokana kukosa zana za kujisitiri, pindi wawapo katika hedhi.
Wakati huo huo, pamoja na serikali, wadau mbalimbali kupinga vitendo vya
kikatili dhidi ya wanawake hasa watoto wa kike katika jamii, bado
imeshindwa kutoa elimu kuhusu mila kandamizi zinazochangia kukwamisha
ndoto zao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya
Mwanamke Duniani, mwakilishi wa Mradi wa Vijana kwa Mabadiliko, Nehema
Nemno, alisema wanaungana na wanawake wengine duniani kuwakumbusha
watoto wa kike umuhimu wa matarajio yao ya badaye.
Alisema watoto wa kike wanapaswa kuandaliwa kwa kuzitambua haki zao hasa
kuhusu afya ya uzazi, madhara ya ukeketaji pamoja na ndoa za utotoni.
“Watoto wa kike baadaye atakuwa mama wa watoto, hivyo akielekezwa na
kuzifahamu athari na faida ya jambo anaweza kuondokana katika mila
kandamizi zinazokwamisha mfumo wa maisha yake kiujumla,”alisema Nemno.
Naye mwakilishi kutoka Shirika la Plan International Tanzania (Plan),
Emmanuel Mang’ana, alisema mradi huo uko chini ya shirika hilo,
ukijulikana kwa jina la Binti Jitambue, na umekusudia kuwalenga vijana
wenye umri wa rika la miaka 16 na kuendelea.
Mkuu wa shule ya Sekondari ya Jangwani, Mwani Senga, alisema msichana
ili kufika malengo yake anatakiwa kusimama kupigania ndoto zake, hivyo
licha ya changamoto nyingi kuliandama kundi hilo, bado nguvu kazi
ikielekezwa linaweza kuondokana na adha linalokumbana nazo mara kwa
mara.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment