Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, amesema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanaendelea kupambana dhidi ya mbinu chafu zinazotumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Alizitaja mbinu hizo kuwa ni kuahirisha uchaguzi huo mara tatu bila
sababu za msingi ikiwamo kisingizio cha zuio la Mahakama kwa ajili ya
uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 26 ambalo limebainika kuwa
halikuwa halali.
Waitara aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kivule
mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuwashukuru wananchi hao kwa kumchangua
kwa kura nyingi, hivyo kuwa miongoni mwa wabunge 10 nchini waliopata
kura nyingi.
Alisema iwapo juhudi zao za kumpata meya wa Jiji la Dar es Salaam
zitafanikiwa, kazi ya kwanza itakuwa ni kuhakikisha wanafuta sheria ya
kuwazuia bodaboda wasiingie mjini na kutumbua jipu la mradi wa mabasi
yaendayo haraka (Darts) kusuasua.
“Hatuwezi kuachia nafasi hiyo kwani CCM wakiipata utekelezaji wa
majukumu ya kuleta maendeleo kwa jamii kupitia Ukawa utakuwa mgumu,
hivyo lazima tuvuke vikwazo vyote,” alisema.
Alisema nafasi ya meya wa Jiji ni muhimu kwa kuwa ndiyo nafasi pekee
inayoratibu itifaki za viongozi wa nchi, hivyo CCM hawapendi mpinzani
apewe jukumu hilo na ndiyo sababu wanatafuta kila sababu kupunguza kasi
ya Ukawa.
Aliongeza kuwa itakuwa ndoto kwa CCM kushinda kwa kura kwenye uchaguzi
wa meya wa Jiji kwa kuwa ina wajumbe 76 wakati Ukawa ina wajumbe 87,
hivyo ipo tofauti ya wajumbe 11.
Aidha, Waitara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule,
alisema wananchi wakiona Mbunge wa upinzania anapigiwa makofi na chama
tawala wafahamu ni msaliti na anapaswa kufukuzwa.
“Nyote mtakuwa mashahidi, nilivyokamatwa na polisi kisha kuwekwa lupango
kwenye sakafu aliyolala Masamaki, lakini nilipofika mahakamani
nilijidhamini mwenyewe, kiukweli sijampiga RAC (Katibu Tawala wa Mkoa),”
alisema.
Mmoja wa wakazi hao, Juma Hamis, alisema wanashukuru kupata taarifa
kutoka kwa mbunge wao, lakini wao wanahitaji maendeleo ya kuboreshewa
miundombinu ya barabara, maji na umeme.
“Tumechoka na ahadi za wanasiasa, tunahitaji vitendo kuliko maneno,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment