Loading...

CWT kuwapa walimu kiinua mgongo.


Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeanzisha utaratibu wa kuwapa mkono wa heri wanachama wake wanaostaafu, utaratibu ulioanza Julai Mosi, mwaka jana, imefahamika.
 
Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch, alisema  jana jijini Dar es Salaam kuwa watakaopewa mkono wa kwaheri  ni  waliochangia chama hicho kwa zaidi ya  miaka 15.
 
Alisema katika kipindi  cha kati ya Julai Mosi na  Desemba, mwaka jana, Sh. milioni 265 zilitumika  kutoa mkono huo kwa wastaafu 781 na kwamba mwaka huu zimetengwa Sh. bilioni 1.4 kwa ajili ya kuwaaga wastaafu 4,200.
 
Aliongeza kuwa  kwa kuanzia,  wastaafu hao  kila mmoja atapewa mabati 20  ya geji 30  yenye urefu wa futi 10.
 
Oluoch  ambaye ni  Naibu Katibu Mkuu wa CWT, alisema utaratibu huo umetolewa kutokana na kikao kilichofanyika  Januari,  mwaka jana, na  kwamba wanachama waliostaafu kuanzia Julai Mosi, ambao wana sifa ndio watakaonufaika.
 
Alisema mkono huo wa kwaheri unaweza ukaboreshwa zaidi baadaye na kwamba badala  ya kuwapatia mabati, inawezekana  chama kikatoa   pikipiki au hata gari kulingana na  uwezo.
 
“Huo ni uamuzi wa kikao hicho kwa hiyo  mwanachama  aliyestaafu kabla ya tarehe hiyo mfano Juni 31, 2015, hataagwa hivyo watabaki kuwa wanachama kwa mujibu wa katiba,”alisema.
 
Alisema chama hicho ambacho ni cha wafanyakazi walimu na si  mfuko wa hifadhi ya jamii  kulingana na katiba yake, hivyo   kitaendelea  kuwatetea  walimu wote waliostaafu na walioko kazini.
 
Miongoni mwa haki hizo  ni kuhakisha  wanapata mishahara  stahiki, viinua mgongo na  matibabu.
 
Mwaka 2009, chama hicho kilikusanya Sh. bilioni 1.2 kutokana na kodi ya pango ya kitega uchumi cha Mwalimu House. Kutokana na mapato hayo, kila  chama cha kuweka na kukopa cha walimu (Saccos)  kutoka  kila mkoa, kilipatiwa Sh. milioni 40. 
 
Walimu wanachukua mikopo kwenye  Saccos hizo na kurudisha asilimia 50 fedha  zote za mkopo.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top