Loading...

Shule bubu isiyo na mtaala kufundishia wala walimu.

Zaidi ya wakazi 5,000 wa jamii ya wafugaji wa Kimasai katika Kijiji cha Kichangale, Simanjiro mkoani Manyara, wamemkodi mwananchi mwenzao kama mwalimu, kufundisha watoto wao kusoma na kuandika.
 
Wananchi hao wamefikia hatua hiyo, baada ya kukosa shule kwa zaidi ya miaka mitano.
 
Mwananchi huyo ambaye hana taaluma ya ualimu, anawafundisha watoto hao bila kutumia mtaala wa elimu wala mwongozo wa serikali.
 
Kutokana ukosefu wa shule na walimu, wanafunzi hao sasa wanashindwa kufaidika na matunda ya elimu bure iliyotangazwa na Rais John Magufuli.
 
Wananchi hao wameeleza kuwa wamekodi Lilian Nanyaro ili awafundishie watoto wao kwa malipo ya Sh. 3,500 kwa mwezi kwa kila mtoto.
 
Licha ya kufundishwa bila kutumia mtaala wowote wa elimu, pia watoto hao wanasoma nyumbani kwa Liliani chini ya mti wa asili huku wakiwa wamekaa chini.
 
Kijiji hicho ambacho kinakaliwa na jamii ya wafugaji, kiliandikishwa kisheria miaka mitano ikliyopita, lakini hakijawahi kupata haduma ya shule wala zahanati.
 
Wakati wanafunzi wakiwa wanafundishwa katika mazingira hayo, wanawake wanapatiwa huduma ya kujifungua mara mbili kwa mwezi ndani ya nyumba ya udongo ambayo imewekewa kitanda cha miti.
 
Kijiji cha jirani na hapo ambacho kina huduma ya shule na zahanati, kiko umbali wa zaidi ya kilomita  25,  hivyo kuwafanya wazazi kushindwa kuwapeleka watoto wao huko kwa ajili ya kusoma kwa kuwa eneo hilo lina wanyama wakali.
 
Akizungumza na Nipashe,  Lilian alisema aliombwa na wananchi hao ili walau awafundishie watoto wao wajue kusoma na kuandika.
 
Alikiri kutotumia mtaala wowote wa elimu unaotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na wala hafuati mwongozo, na badala yake anachokifanya ni kujaribu kuwafundisha ili wajue kusoma na kuandika tu.
 
Aliongeza kuwa kuna mwitikio mkubwa wa wafugaji hao kupeleka watoto wao shule na kwamba anafundisha zaidi ya watoto 100 chini ya mti na wengine ameshindwa kuwapokea kutokana na mazingira mabovu ya kuwafundishia.
 
Miongoni mwa mazingira hayo ni pamoja na kukaa chini, ukosefu wa choo, na tatizo la njaa kwa watoto hao.
 
Mwenyekiti wa kijiji hicho,  Joseph Lekele, alisema tayari wananchi wameanzisha mpango maalumu kwa ajili ujenzi wa shule ya msingi.
 
Alisema wananchi wameanza kukusanya mawe na mchanga na kumwomba Rais Magufuli awahimize watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kuwasaidia ili wapate shule pamoja na walimu.
 
''Hapa kijijini tunateseka sana. Sisi wafugaji tunaona kama tumetengwa kwa kuwa watoto hawana shule ya kusoma kama unavyowaona wanafundishwa kienyeji chini ya mti,'' alisema.
 
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Komoro, Japhet  Losinyaki, alisema wananchi wa kijiji hicho wanakabiliwa na tatizo kubwa la shule na kwamba wamejitolea kukusanya mawe na mchanga ili kujenga shule.
 
Akizungumza na Nipashe,  Mratibu wa Elimu Kata ya Komoro, Dismas Laswai, alikiri Lilian kufundisha watoto hao bila kufuata mtaala wowote wala muongozo wa elimu.
 
Aliiomba serikali kukitazama kijiji hicho kwa kuwa watoto wao wanapata shida kutokana na ukosefu wa shule, hatua ambayo inawafanya washindwe kusoma.
 
Mwenyekiti wa shirika lisiolo la serikali la 92  Foundation la jijini Dar es Salaam, ambalo limeanzisha harakati za kuisaidia jamii ya Kimasai kupata elimu, Muganyizi Ernest, alisema wameanza kufanya mipango mbalimbali inayolenga kuwasaidia wananchi hao.
 
Alitaja baadhi ya mipango hiyo kuwa ni pamoja na kuandaa hafla ya kuchangisha fedha, itakayoshirikisha wadau mbalimbali, wakiwamo viongozi wa serikali.
 
Alisema mipango ya awali imekamilika kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo na kuiomba serikali kuweka nguvu zake kwa kuwa jamii ya Kimasai inapata shida kutokana na ukosefu wa shule na zahanati.
 
Akizungumzia tatizo hilo ambalo linaikumba jamii ya Kimasai, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera, alisema yeye pamoja na serikali yuko tayari kuhakikisha shule inapatikana katika kijiji hicho.
 
Hata hivyo, alikiri kwamba hajawahi kufika kijijini hapo. Ameahidi   kulishughulikia tatizo hilo.
 
"Nitamwambia Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro ahakikishe anafika hapo ili aangalie namna ya kuwasaidia wananchi hao waweze kupata shule," alisema.
 
Alisema yuko tayari kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho ili kuona namna ya kupata fedha na maandalizi ya kujenga shule hiyo.
 
Bendera alisema kama kijiji hicho hakina shule lazima ijengwe na kwamba hakuna namna nyingine ya kukwepa hilo na kusisitiza kwamba lazima kila mtoto aende shule.
 
Bendera alisema inasikitisha kuona watoto wengine wanafaidi matunda ya elimu bure huku wenzao wakiyakosa na kwamba atahakikisha anafuatilia suala hilo haraka.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top