Wasomi wanena, kivuli cha Lowassa chaitesa CCM.
Joto la uchaguzi wa mwaka 2015 kuanzia ndani ya vyama, lilifanya Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujitoa CCM na kujiunga na Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hatua hiyo ilizidisha joto hilo na matokeo yake vyama vya upinzani
vikapata takribani wabunge 110 na takriban halmashauri 25, idadi ambayo
haijawahi kufikiwa na vyama vya upinzani.
Baadhi ya Halamashauri ambazo hazijawahi kuwa chini ya upinzani na
kutokana na nguvu ya Ukawa kwenye uchaguzi uliopita ilizichukua ni zile
za Tanga mjini na Dar es Salaam kwa manispaa za Kinondoni na Ilala.
Mbali na kuwa na madiwani wengi na kufanikiwa kuongoza Halmashauri za
Ilala na Kinondoni, huku vikikosa Temeke, bado vyama vya CUF na Chadema
ambavyo vyote viko chini ya Ukawa, vinaizidi CCM takribani madiwani 10
kwa jiji la Dar es Salaam, hivyo kuwapa uwezekano mkubwa wa kuongoza
halmashauri ya jiji pia.
Wakati wa kampeni, maeneo ambayo Lowassa aliweka nguvu kubwa kwa
kufanya mikutano mingi ni pamoja na Dar es Salaam na Tanga mjini,
matokeo yake Ukawa iliibuka na ushindi mkubwa.
Baada ya mameya wa Ilala na Kinondoni kutangazwa na kwenda nyumbani kwa
Lowassa kumshukuru, moja ya mitihani aliyowapa ni kuhakikisha jijini
linakuwa la mfano kwenye maendeleo na kutumikia wananchi.
Miezi minne sasa baada ya uchaguzi mkuu, uchaguzi wa meya wa jiji la Dar
es Salaam umekuwa na vitimbi vilivyofanya mpaka sasa uahirishwe mara
tatu kutokana na sababu zisizoelezeka.
Kwa jiji la Tanga, upinzani wana madiwani 17 na CCM 12, hatua ambayo
imesababisha halmashauri kushindwa kufanya kazi, baada ya CCM kushinda
kiti cha umeya na upinzani kukataa kwa madai kwamba haki haikutendeka.
Hali iko hivyo hivyo kwenye wilaya ya Kilombero ambako pia uchaguzi
uliahirishwa mara kadhaa kabla ya kufanyika tena wiki hii na CCM kuibuka
mshindi, licha ya upinzania kuwa na madiwani wengi. Hatua hiyo
ilisababisha kuwapo malalamiko kwamba kuna mbinu chafu zilifanyika.
Halmashauri zingine ambazo vyama vya Ukawa vilikuwa na madiwani wengi ni
Kilimanjaro kwa wilaya za Hai, Rombo, Moshi, Siha na manispaa ya
Moshi.
Mbeya ni jiji la Mbeya Mji Tunduma; Arusha- jiji la Arusha, Monduli na
Arumeru; Manyara-Karatu na Mji Babati, Kagera-Manispaa ya Bukoba na mji
mdogo wa Kayanga.
Kwa upande wa Mtwara, vyama hivyo vilikuwa na madiwani wengi Tandahimba,
Mtwara/Mikindani, Mji Newala, Lindi (Kilwa), Tanga (Jiji Tanga), Mara
(Serengeti, Tarime na Mji Tarime), Morogoro-Kilombero na Ifakara huku
katika Mkoa wa Iringa kukiwa na madiwani wengi kwenye Manispaa ya
Iringa.
Mkoani Kigoma, Ujiji/ Kigoma inaongozwa na ACT –Wazalendo ambao si
sehemu ya Ukawa. Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, halmashauri hiyo
ilikuwa na madiwani wengi kutoka Chadema.
Migogoro hiyo ambayo matokeo yake ni kukwama kwa shughuli za halmashauri
husika, baadhi ya wadau wanasema wananchi ndio wanaoumia zaidi.
SAMIA ATABIRI MDORORO
Akizungumza na viongozi serikali na kisiasa jijini Tanga hivi karibuni,
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema serikali italazimika
kuivunja halmashauri ya jiji hilo endapo mgogoro uliopo hautamalizwa
haraka.
Kauli hiyo ilitokana na kushindwa kufanyika kwa vikao vya maendeleo vya
halimashauri hiyo kutokana na mgogoro wa kisisa baina ya CCM na vyama
vinavyounda Ukawa, ambavyo ndivyo vyenye madiwani wengi, vikituhumu
chama tawala kutumia mabavu kushinda uchaguzi.
“Mpaka sasa jiji la Tanga hakuna uongozi uliosimama. Sasa hatuwezi
kwenda kwa mwendo huu, wananchi wanahitaji maendeleo na kurudia uchaguzi
hatuwezi ni gharama kubwa. Kilichobaki ni kuivunja halmashauri mpaka
hapo muda wa kufanya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya nchi utakapotimia,
hivyo kwa maana nyingine kama itavunjwa serikali kuu ndiyo itasimamia
shughuli za jiji hili.
“Jiji ni kioo cha mkoa mzima, sasa kama wazee hawatakaa kitako na
viongozi kutafuta suluhu, basi hii mipango yenu yote ya kufufua viwanda
itakuwa ndoto tu kwa sababu hapa mjini hakupo shwari na tunalitambua
hilo,” alisema.
MEYA TANGA AANZA KUJUTA
Meya wa Jiji la Tanga, Mustapha Mhina, aliliambia gazeti hili kuwa
kuvunjwa kwa halimashauri hiyo kutawaathiri zaidi wananchi ambao
wanalitegemea zaidi Baraza la Madiwani katika usimamizi na utatuzi wa
kero zinazowakabili.
Alipohojiwa na Nipashe, Mhina alisema kuvunjwa kwa Halmashauri kwa maana
nyingine ni kutengua nafasi aliyo nayo diwani katika usimamizi wa
miradi, matumizi ya fedha na msukumo wa utetezi wa kero za wanachi
kutoka kwa watendaji .
Alisema iwapo serikali itachukua uamuzi huo, haina budi kutambua kwamba
watendaji watakuwa wasimamizi na wafanyaji wa uamuzi wowote, jambo
ambalo wakiwapo wasio waaminifu huweza kutumia mwanya huo kujinufaisha
badala ya kuwaondolea wananchi kero zinazowakabili.
Hata hivyo, aliwataka madiwani wa CUF kukubali kukaa kwenye meza ya
mazungumzo ili kukamilisha ajenda zilizobaki wakati wa kikao
kilichovunjika Desemba, mwaka jana, baada ya Msimamizi wa Uchaguzi
kumtangaza mshindi wa nafasi ya Meya.
Kwa mujibu wa Mhina, ajenda zilizobaki ni pamoja na ile ya kuchagua
kamati za kudumu za halmshauri, kupitisha ratiba za vikao, kupokea
taarifa ya utendaji wa halmashauri katika kipindi madiwani walipokuwa
kwenye uchaguzi na kusomewa taarifa ya serikali.
Alisema Baraza hilo halikufanya kikao rasmi kwa mujibu wa sheria na
kanuni kwa kuwa mpaka sasa hakuna barua waliyoipokea kutoka kwa
Mkurugenzi wa Jiji ya kuitwa kwenye kikao.
“Ukifuata kanuni na sheria ni kwamba kama Baraza litashindwa kukutana
katika vikao vitatu litavunjwa. Lakini sisi hatujakaa hata kimoja, sasa
niwaombe wenzetu waliangalie jambo hili kwa kina sana kuwa sisi ni
wamoja na ni wana Tanga na kwamba kuna maisha baada ya siasa.
Hao watakaovunja halmshauri hawawezi kuwa na uchungu kama tulio nao
sisi,” alisema Mhina ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nguvumali.
KIGOMA WACHANJA MBUGA
Wakati migogoro ikiendelea kwenye Halmashauri hizo, Mbunge wa Kigoma
Mjini, Zitto Kabwe, alisema kutokana na amani kwenye Halmashauri ya
Manispaa ya Kigoma/Ujiji inayoongozwa na ACT-Wazalendo, tayari wameanza
kufanya kazi za wananchi.
Zitto alisema pamoja na mambo mengine wamefanya mazungumzo na wadau
balimbali na wana mpango wa kuanzisha bima ya afya kwa wananchi wote na
mpango maalumu wa kuhakikisha wanaboresha elimu ili shule za jimbo hilo
zisifanye vibaya kama ilivyokuwa kwenye mtihani uliopita wa kidato cha
nne.
Alisema lengo ni kuhakikisha Kigoma/Ujiji inakuwa halmashauri ya mfano kwa kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Hali ya migogoro kwenye halmashauri hizi ni kama ile iliyokuwa Bukoba
Mjini, awamu iliyopita kutokana na mgawanyiko ndani ya baraza la
madiwani. Mgogoro huo ulisababishwa na aliyekuwa Meya, Anatory Amani na
Mbunge, Balozi Khamis Kagasheki na ule wa Arusha ambao ulitengamaa baada
ya miaka kadhaa.
Halmashari ya Manispaa ya Bukoba kwa takribani miaka mitano ilishindwa
kufanya mradi wowote wa maendeleo, kutokana na kutofanyika kwa vikao
ambavyo pamoja na mambo mengine vinatakiwa vipitishe bajeti za
maendeleo.
Hali hiyo pia inanukia kwa jiji la Dar es Salaam ambalo mpaka sasa
halijafanya chochote kutokana na kutokuwa na uongozi, Tanga na Kilombero
hali ikiwa vivyo hivyo.
KILICHOWAPATA ARUSHA
Pia Arusha ilikuwa na mgogoro kwenye awamu iliyopita kutokana na Mbunge
wa sasa wa Arusha mjini, Godbless Lema, ambaye pia alikuwepo kipindi
kilichopita, anasema mambo mengi yalikwama kutokana na mtafaruku huo.
"Kama mnakumbuka uchaguzi wa mwaka 2010 wakati wakimchagua Meya wa Jiji
la Arusha, kulitokea vurugu zilizosababisha mauaji ya watu wasio na
hatia ubabe ukafanyika Meya akapatikana, kila mtu alijua kilichofanyika
na athari zake ni kubwa,” alisema.
“Kwa mtizamo huo vikao havikuwa na amani, madiwani walikuwa na migogoro,
mambo ya msingi ya maendeleo ambayo yaliletwa na Chadema au CCM ili
yajadiliwe yalikwama,” alisema.
Alisema athari zingine zinazotokana na migogoro hiyo ni kujengeka uadui
baina ya wananchi na serikali yao kwa kuamini kuwa uamuzi wao wa
kumchagua kiongozi fulani haujaheshimika.
Pia alisema athari nyingine ni vikao vya kujadili mambo ya maendeleo havifanyiki badala yake kunakuwa na vile vya malumbano.
Pia alisema migogoro hiyo inaleta madhara kwa wafadhili kwa sababu
kutoka uchaguzi mkuu uishe kinachoendelea baadhi ya majiji ni malumbano
ya nani awe meya badala ya kuzungumzia maendeleo.
BUKOBA WALIVYOSOTA
Kutokana mgogoro wa madiwani wa Manispaa ya Bukoba katika awamu
iliyopita, miradi ya maendeleo haikutekelezwa kwa sababu vikao vilikuwa
havifanyiki.
Manispaa hiyo ilitegemea kupata michango ya wahisani lakini haikutolewa
kwa sababu waliposikia kuna migogoro walikimbia hivyo kutotimia kwa
malengo waliyokuwa wamepanga kuyatekeleza.
WASOMI WALONGA
Baadhi ya wasomi waliozungumza na gazeti hili, walisema athari za migogoro inayoendelea sasa itaonekana zaidi kwa wananchi.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Dk. Kitojo Wetengere, alisema ni aibu
kuwapo migogoro kwenye baadhi ya halmashauri ilhali kuna sheria
zinazoongoza uchaguzi na mambo yote ya halmashauri.
Alisema uchaguzi wa Meya wa Halmashauri uko kwa mujibu wa sheria na
taratibu zilizowekwa lakini watu wachache wenye malengo yao binafsi
wamekiuka taratibu hizo.
“Haiwezekani serikali iweke sheria, kanuni na taratibu lakini watu
wachache ambao wameona kwa sababu wanazoamini wao, wavuruge uchaguzi na
kuendelea kuwachwa,” alisema.
Kuhusu athari ambazo zinatokana na kuahirishwa kwa uchaguzi huo, alisema
ni watu kuathirika kisaikolojia na kufikiria uchaguzi wa Meya na
matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wakati watu walishamaliza
badala ya kufikiria shughuli za kufanya.
Alisema matokeo ya hayo ni kukaribisha makundi ya siasa kuanza kushamiri
badala ya vijana kufikiria kufanya kazi na kusukuma gurudumu la
maendeleo.
Naye Mhadhiri wa Idara ya Sayansi za Siasa na Utawala kutoka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Rasul Ahmed, alisema tatizo kubwa
linalojitokeza ni vyama shiriki kutokukubali kushindwa.
“Sioni kama ni jambo la ajabu wajumbe wa chama fulani kumpigia kura wa
chama kingine na akashinda uchaguzi huo, jambo ambalo wengi wanadhani
haliwezekani na ndio sababu vyama havijajiandaa kushinda,” alisema.
Alisema bado hakuna ukomavu wa kisiasa kutokana na vurugu zilizotokea na
kuahirishwa kwa uchaguzi katika Halmashauri za Kilombero, Tanga na Dar
es Salaam.
Alisema vurugu ambazo zimetokea, zimeirudisha nyuma hatua tano
demokrasia ya Tanzania na kusababisha wananchi kugawanyika kutokana na
vyama vyao kuwaangusha.
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, alisema tatizo
kubwa linalojitokeza Kilombero, Tanga, Dar es Salaam na Zanzibar ni
kutokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutojiandaa kushindwa.
Alisema CCM haijakubali kuwa iko kwenye mfumo wa vyama vingi na kutokana na hali hiyo, chama chochote kinaweza kushika dola.
Alisema athari kubwa ambayo itatokea ni watu kuchoka na kuamua kufanya jambo lolote ambalo linaweza kuwa na athari kwa nchi.
Lipumba alimshauri Rais Dk. John Magufuli kuingilia kati ajenda ya kidemokrasia ambayo inamalizwa na watu wachache.
Alisema ni vyema pia akaagiza uchaguzi wa meya ufanyike na mshindi apatikane ambaye ataongoza katika halmashauri hiyo.
Habari hii imeandaliwa na Romana Mallya, Mary Geofrey, Dar, Na Lulu George, Tanga na Lilian Lugakingira Bukoba.
Post a Comment