Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (pichani), ameiagiza Kamati ya Uchumi ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu ikutane na wafanyabiashara wote ili wajadiliane na kupanga kiwango cha ushuru kinachopaswa kutozwa kwenye mazao ya wilaya hiyo.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana, wakati akizungumza na mamia ya
wananchi waliofika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja
wa michezo wa Dutwa, wilayani hapa.
Alitoa agizo hilo baada ya kuona bango lililoshikwa na wananchi
wakilalamikia kutozwa ushuru wa Sh. 3,000 kwa gunia moja la mazao badala
ya Sh. 1,000 ya zamani.
Alisema masuala ya ushuru ni maamuzi baina yao na Halmashauri, lakini
hiyo tozo imeongezwa sana, hivyo kuagiza kamati hiyo na wafanyabiashara
wakutane kujadili suala hilo na wakubaliane kiwango cha ushuru.
Alisema: “Wabunge pia waalikwe kwenye kikao hicho na Mwenyekiti wa
Halmashauri pamoja na Baraza la Madiwani nalo pia lishiriki. Kama
mnataka kupandisha ushuru ni lazima mkubaliane viwango ili Watanzania
wafanye biashara wakiwa na mapenzi na nchi yao.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema suala la kulipa ushuru ni la muhimu
katika kuchangia makusanyo ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
“Ushuru ni lazima ulipwe, lakini pia ni lazima muwe mmekubaliana ni
kiwango gani mnatoza,” alisema Majaliwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewazuia maofisa kutoza ushuru na
kudai fedha kabla mwananchi hajauza mifugo wanapoipeleka mnadani akisema
kuwa wanakuwa wamekwenda kutafuta fedha.
Alifanya uamuzi huo wakati akijibu hoja iliyotolewa na Mbunge wa Viti
Maalum (Chadema), Gimbi Masabo, ambaye alimweleza Waziri Mkuu kwamba
kuna tabia ya kutoza Sh. 6,000 kwa kichwa kwa kila ng’ombe anayeswagwa
kuingia eneo la mnada bila kujali kama mtu huyo ameuza ng’ombe au la.
Alimwagiza Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Robert Lweyo, aimarishe
usimamizi wa minada na kujua idadi ya mifugo ambayo inaingizwa,
inayouzwa na ile inayobaki ambayo imeshindikana kuuzwa.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment