Serikali imekiri udhaifu kwa shule zake kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa, huku ikijitetea kuwa za binafsi zinafanya vyema kwa sababu zinaiba walimu waliosomeshwa na serikali na kuwalipa fedha nyingi.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa wiki chache baada ya Baraza la Taifa la
Mitihani Tanzania (Necta), kutangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha
nne. uliofanyika Novemba. mwaka jana. huku shule zzake zikifanya vibaya
kuulinganisha na za binafsi.
Kamishna wa Elimu katika Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi,
Prof. Eustella Bhalalusesa, alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa
akizungumza na Nipashe. Gazeti hili lilitaka kujua sababu ya shule za
serikali kufanya vibaya.
Prof. Bhalalusesa alisema sababu ya walimu hao kushawishika na kukubali
kwenda kufundisha shule binafsi, ni kutokana na mishahara wanayolipwa
kuwa mikubwa na kwamba serikali haiwezi kuimudu.
Wakati kamishna huyo akieleza hayo, matokeo ya kidato cha nne
yaliyotangwaza wiki mbili zilizopita, yanaonesha shule za serikali
zimeendelea kushika mkia.
Katika matokeo hayo, shule za serikali ambazo ni za watoto wenye vipaji
maalumu zilizokuwa zimezoeleka kufanya vizuri, hazikufua dafu kutokana
na Ilboru kushika nafasi ya 53, Kibaha (69), Mzumbe (71) na Kilakala
nafasi ya 94.
“Hawa wenzetu wamewekeza na unakuta ada ya mtoto mmoja pekee ni Sh.
milioni tisa sasa unafikiri watashindwaje kumchukua mwalimu kutoka
serikalini pindi wanapomtaka? Walimu tunaobakia nao ni wazalendo pekee,”
alisema.
Prof. Bhalalusesa alisema sababu nyingine ni shule za serikali kuchukua
wanafunzi wa kawaida wakati za binafsi huchukua walio bora.
Alisema wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza shule za serikali na wale
wa binafsi wanatofautiana, ndiyo maana matokeo yanapotoka wao hufanya
vizuri zaidi.
“Ila kwa kidato cha sita, matokeo huwa tofauti kwa sababu hawa tayari
wamechujwa na mitihani ya kidato cha nne, kwa hiyo ufaulu wao huwa mzuri
zaidi,” alisema.
Kuhusu mikakati ya serikali katika kuziboresha shule hizo, Prof.
Bhalalusesa alisema katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2016/17,
baadhi ya shule hizo zitakarabatiwa.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment