Serikali imesema inatarajia kuondoa kitengo cha kupeleka wagonjwa kutibiwa nje ya nchi na badala yake imepanga kuziwezesha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa ya Moi na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kuzitengea fedha ili zitoe huduma zote.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Khamis Kigwangalla, alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa wodi ya wagonjwa chini ya uangalizi maalum (ICU) na vitanda ambavyo vimefadhiliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Gastrenterology Foundation ya Ujerumani.
Dk. Kigwangalla alisema mipango ya kuondoa kitengo hicho imeanza na wanaamini si zaidi ya mwaka mmoja watakuwa wamekamilisha.
Alisema kwa kuwa taasisi hizo zitakuwa zimewezeshwa, endapo kutatokea kuna mojawapo ikashindwa kuwahudumia wagonjwa wake na kutakiwa kuwapeleka nje ya nchi kwa matibabu zaidi, serikali haitahusika tena kugharimia chochote isipokuwa ghamara zitaihusu taasisi husika.
“Tuko katika mkakati wa kuondoa kitengo cha kupeleka wagonjwa kutibiwa nje ya nchi.Tunatarajia kuziwezesha taasisi zetu za Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Moi,” alisema na kuongeza:
“Kitengo kitakachoshindwa kutibu wagonjwa wake, kitagharimia chenyewe kupeleka mgonjwa wake nje ya nchi."
Dk. Kigwangalla alisema tayari taasisi ya Moyo ya JK nayo imeonyesha mafanikio kwa kutoa huduma za moyo ambazo awali zilikuwa zinatolewa nje ya nchi.
Alisema kuanzia Juni, mwaka jana hadi Januari, mwaka huu, taasisi hiyo imetibu wagonjwa 92 wa moyo kati ya 100 waliopelekwa kupatiwa huduma hiyo.
“Taasisi ya Moyo ya JK ina kila kitu na imeonyesha uwezo mkubwa, hivyo tunaamini zikiwezeshwa zaidi zitatoa huduma nzuri na hakutakuwa na wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi tena,” alisema Dk. Kigwangalla.
Kauli hiyo ya Dk. Kigwangalla inafuatia Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, aliyesema serikali kuanzia kipindi cha Januari hadi Desemba, mwaka jana ilikuwa inadaiwa Sh. bilioni 29 kutokana na kupeleka wagonjwa nje ya nchi kutibiwa magonjwa ya moyo.
Mwalimu alisema licha ya kupunguza kasi ya kupeleka wagonjwa hao nje, lakini bado inakabiliwa na vifaa vya kisasa vya upasuaji.
Aidha, Dk. Kigwangalla alisema bado kuna uhaba wa vitanda na madaktari wa kuhudumia kitengo cha ICU na kuuagiza uongozi wa Muhimbili kuhakikisha inaangalia uwezekano wa kuogeza madaktari hao haraka.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, alisema awali hospitali hiyo ilikuwa na vitanda vinane tu vya kulaza wagonjwa wanaohitaji huduma maalum, lakini baada ya kupatiwa msaada huo wamepata vitanda 25.
Hata hivyo, alisema bado lengo halijafikiwa kwa kuwa vitanda vinavyohitajika ni 1,500 vya kulaza wagonjwa hao.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment