Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea, amepanda kizimbani na kukanusha kutoa lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Kubenea aliyasema hayo jana kwenye mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Katika utetezi wake alioanza kuutoa jana, Kubenea alidai kuwa siku ya
tukio, Makonda alimzuia kuzungumza na wananchi waliokuwa wamemwita,
akidai kwamba yeye Rais wa Kinondoni na ameshazungumza, hivyo hakuna
ruhusa ya mtu mwingine kusema.
Akiongozwa na wakili wake, Peter Kibatala, Kubenea alidai: "Mheshimiwa
hakimu, mimi sijatamka maneno hayo kwamba Makonda ni mjinga, mpumbavu,
kibaka na cheo chenyewe cha kupewa bali nilimwambia wewe umeteuliwa na
rais na mimi nimechaguliwa na wananchi… ndipo akaniambia yeye ni rais wa
Kinondoni akishaongea hakuna ruhusa ya mtu mwingine kuongea."
Kubenea alidai kuwa Desemba 14, 2015 katika kiwanda cha TOOKU Garments
Co. Ltd, kilichoko Mabibo External, Ubungo, wakati wa mgomo wa
wafanyakazi wa kiwanda hicho alimwambia mkuu huyo wa wilaya kwamba
hawezi kufunga mkutano bila yeye mbunge kuzungumza kwa sababu ni
mwakilishi wa wananchi.
“Makonda alinijibu kwamba kila anapozungumza yeye ndiye mtu wa mwisho
kwa sababu ni rais wa Kinondoni anachokiamua hakuna kingine” alidai
Kubenea.
Akifafanua zaidi, mshtakiwa alidai kuwa alimweleza Makonda kwamba yeye
ni mbunge na amechaguliwa na wananchi kwa zaidi ya kura 17,000 hivyo ni
lazima aheshimu uwapo wake katika tukio hilo.
Alidai pamoja na kujieleza kwamba aliitwa na wananchi kwenye mkutano
huo, DC Makonda hakumpa nafasi ya kuzungumza na badala yake alimwamuru
Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Polisi Magomeni, Denis Mujumba, kumkamata
apelekwe kupumzishwa.
“Kamanda Mujumba alinifuata na kunieleza kwamba niko chini ya ulinzi.
Aliniamuru ninyooshe mikono, nilimhoji ananikamata kwa kosa gani au kwa
kuagizwa na mkuu wa wilaya?” alidai Kubenea.
Pia DC (Mkuu wa Wilaya) Makonda aliamuru raia wa China anayedaiwa kunyanyasa wafanyakazi hao akamatwe na achunguzwe.
Awali, Kubenea alidai mahakamani hapo kuwa siku ya tukio, majira ya saa
tano asubuhi, alifika kwenye kiwanda hicho, baada ya kupata taarifa za
kuwapo kwa mgomo na wakazungumza hadi saa 9.30 jioni.
Alidai akiwa kiwandani hapo alionana na uongozi wa kiwanda hicho,
uongozi wa chama cha wafanyakazi juu ya madai mbalimbali ikiwamo
nyongeza ya mshahara na kwamba wakakubaliana kuongeza asilimia tano toka
Sh 100,000.
Alibainisha kuwa wakiwa bado katika mkutano huo, walisikia ving'ora na
wafanyakazi waliokuwapo nje wakiamini ni Rais Dk. John Magufuli
amekwenda kimbe ni Makonda ameongozana na askari polisi ambao idadi yao
hawezi kuikumbuka.
Kubenea alidai kuwa alitambia uwapo wake, akampa taarifa na mahali
walipofikia na kwamba Mkonda alimweleza kuwa ''Mbunge hawa watu ni
wahuni twende ndani ya kikao tukapambane.
''Tukiwa ndani kikao kilianza upya, muafaka haukupatikana na Makonda
aliahidi kesho yake Desemba 15, 2015 kuwapeleka waziri wa viwanda na
biashara na waziri wa kazi na ajira na akwapa nafasi watu wengine
kuongea yeye akamnyima.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya mashahidi watatu wa upande wa mashtaka
ambao ni Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi, ASP Denis Mujumba (39),
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda pamoja na askari PC Gabriel
kutoa ushahidi wao dhidi ya kesi hiyo inayomkabili Kubenea na kuufunga.
Katika kesi hiyo, Kubenea anadaiwa kuwa Desemba 14, 2015 katika kiwanda
cha Tooku Garments Co.Ltd kilichopo Mabibo External alimtolea lugha ya
matusi DC Makonda kuwa wewe ni kibaka, mjinga, mpumbavu tena
umeteuliwa kwa kupewa.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment