Loading...

Afisa Uchaguzi ahukumiwa kifungo cha Miaka 7 jela kwa Rushwa


Afisa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara Bw.  Julius Bujabhi Makwasa amehukumiwa kifungo cha Miaka 7 jela baada ya kupatikana na hatia ya Makosa 34 yakiwepo ya Rushwa.

Mnamo mwaka 2013 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Mara ilimfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti Afisa uchaguzi wa Halmashauri hiyo Bwana Julius Bujabhi Makwasa na wenzake wawili wakishitakiwa kwa makosa thelathini na manne yakiwemo ya matumizi mabaya ya fedha za umma, kuisababishia hasara Halmashauri ya Serengeti, kusaidia kutenda kosa, kughushi na kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri wao.

Washitakiwa wengine katika shauri hilo la uhujumu Uchumi E.C.C 130/2013 lililokuwa likisikilizwa na Hakimu wa Mahakama hiyo Mheshimiwa Ismail Emanuel Ngaile,  walikuwa  Bi Scola Daudi Mosi ambaye ni mtunza kumbukumbu wa Halmashauri hiyo na Bwana Dickson Julius Makwasa ambaye ni mtoto wa mshitakiwa wa kwanza.

Ilidaiwa na mwendesha mashitaka wa TAKUKURU Wakili Martin Makani mbele ya mheshimiwa Ngaile kwamba mshitakiwa wa kwanza Julius Makwasa  ambaye majukumu yake yalikuwa pamoja na kuviteketeza vifaa vya uchaguzi muda wa uchaguzi unapopita na mshitakiwa wa pili Scola Mossy ambaye  majukumu yake ni pamoja kusimamia kumbukumbu zinazoingia na zinazotoka nje ya Halmashauri hiyo,  kwa nafasi zao hizo,  walikuwa na jukumu la kuharibu nyaraka za uchaguzi mkuu wa Octoba 2010 kama ilivyokuwa imeelekezwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi.

Katika kutekeleza jukumu hilo ilielezwa kwamba, waliandaa majina ya vibarua na kuingiza majina hewa ishirini na tano (25) kuonyesha kwamba majina hayo hewa pia yalishiriki  kuchimba mashimo, kusomba nyaraka hizo za uchaguzi na kuzipeleka kwenye mashimo kisha kuziteketeza kwa moto hivyo kustahili malipo.

Katika udanganyifu huo ilielezwa kwamba, mshitakiwa wa kwanza na wa pili waliweza kuandaa nyaraka za kuipotosha Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kuwawezesha kujipatia jumla ya shilingi million tatu laki nane na elfu hamsini (Tsh 3,850,000/=) kwa kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri .

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top