Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimewasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya ualimu wa sayansi kwa ngazi ya stashahada na kuwataka waondoke chuoni hapo mara moja.
Jana, lilitolewa tangazo chuoni hapo likiwataka wanafunzi hao kuondoka kati ya jana hadi leo saa 12 jioni. Tangazo hilo lilieleza kuwa kutokana na matatizo yaliyopo katika ufundishaji wa stashahada hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imeamua wanafunzi hao kurejea majumbani na wataelezwa mustakabali wao “mapema iwezekanavyo”.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula alipotakiwa kufafanua suala hilo, alisema kwa ufupi kuwa suala hilo lipo lakini akaelekeza apigiwe simu Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Beatrice Baltazal kwa maelezo zaidi.
Baltazal alipotafutwa alisema kusimamishwa kwa wanafunzi hao kulitokana na agizo la Serikali na wametakiwa kulitekeleza.
Kuhusu lini na nini hatima ya wanafunzi hao, alisema bado hawajui hadi hapo watakapoelekezwa vinginevyo.
Hata hivyo, kulikuwa na malalamiko kwa wanafunzi hao juu ya namna walivyopewa taarifa za kusimamishwa masomo yao kwa ghafla na kutakiwa kuondoka.
Kozi ya stashahada ya ualimu wa sayansi, ilianzishwa maalumu kwa agizo la Rais Jakaya Kikwete kwa lengo la kuziba pengo la walimu wa sayansi na ilikuwa inatolewa UDOM pekee.
Waliokuwa na sifa za kujiunga na kupewa mikopo ni wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na kufaulu vizuri masomo ya sayansi.
Wanafunzi hao waliokuwa wamekopeshwa na Serikali wamesimamishwa siku mbili baada ya wenzao zaidi ya 480 wa Chuo Kikuu cha St. Joseph kusimamishwa baada ya kubainika hawakuwa na sifa za kudahiliwa.
Post a Comment