Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 80 (Sh.trilioni 171) zinahitajika katika kukamilisha ujenzi wa miundombinu kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Majaliwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao
cha tano cha Bunge la tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki
kitakachofanyika kwa wiki mbili.
Alisema nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zinahitaji dola za
Kimarekani bilioni 20(Sh.trilioni 42) ili kufanikisha ujenzi wa
barabara, pamoja na dola za Kimarekani bilioni 30 (Sh.trilioni 64) ili
kukamilisha ujenzi na ukarabati wa reli.
Alisema dola za Kimarekani bilioni 10 (Sh. trilioni 15) zinahitajika
katika upanuzi wa bandari, na ujenzi wa bandari mpya, na dola za
Kimarekani bilioni tano (Sh.trilioni 10) zinahitajika kwa ajili ya
ufufuaji wa umeme na miradi mbalimbali ya kuzalishia nishati hiyo.
Kuhusu ujenzi wa reli ya viwango vya kimataifa (Standard Gauge),
Majaliwa alisema ukarabati na upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi wake
umeshaanza kwa baadhi ya nchi.
Alisema nchini Kenya hadi sasa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya
kisasa kutoka mjini Mombasa hadi Nairobi ulishaanza tangu Septemba
mwaka jana na umeshafikia asilimia 40.
Alisema zaidi ya kilometa 200 zimeshajengwa kati ya kilometa 472 zilizopangwa kujengwa.
“Nchi Jumuiya wanachama wa Afrika Mashariki wameshaanza ujenzi wa reli
za kisasa zitakazosaidia usafirishaji wa mizigo kutoka nchi moja kwenda
nyingine,” alisema Majaliwa.
Aliongeza kuwa, nchini Uganda ujenzi wa reli kutoka Tororo-
Pakwach-Gulu-Atiak-Nimule hadi Juba umeanza kufanyiwa tathimini na
wataalam, na kwamba ujenzi wa reli hiyo ulisainiwa na serikali ya Uganda
na Kampuni ya Kichina ya China Habrbour Engineering Company (CHEC)
Machi 30, mwaka jana.
Alisema ujenzi wa reli hiyo unatarajiwa kumalizika mwaka huu,
ikijumuisha ujenzi wa reli kutoka
Malaba-Kampala-Kasese-Bihanga-Kigali-Bujumbula hadi Kisangani.
Alisema kwa upande wa Tanzania, ujenzi wa reli kutoka Uvinza-Musongati
unaendelea na makubaliano ya ujenzi huo yalifanyika Machi mwaka jana
ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli kutoka Dar es
Salaam-Isaka-Keza-Gitega-Musongati ambao upo katika mchakato.
Naye Spika wa Bunge la EAC, Daniel Kidega, alimwapisha mjumbe mpya wa
bunge hilo, Balozi Augustine Mahiga ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje,
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Tanzania.
Pia, Kidega alisifu juhudi na kasi inayofanywa na Rais Dk. John Magufuli
ya uchapakazi na kuwasihi wajumbe wa Bunge la EAC kuiga mfano huo.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment