SERIKALI ya Rais John Magufuli inajidanganya kwamba, inaweza kujiendesha yenyewe kwa kutegemea mapato yake ya ndani. Kwa fikra hizo, itaporomoka tu, anaandika Happiness Lidwino.
Kauli hiyo imetolewa leo na Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo kwenye mahojiano ya moja kwa moja kutoka Dodoma katika Kituo cha Utangazaji cha ITV.
Mbunge huyo amesema, Serikali ya Rais Magufuli inapaswa kwanza kutafuta marafiki ambao wangeweza kumsaidia kusimamisha serikali yake na si kujitenga nao na kwamba, huo ndio mfumo wa rais yeyote anayeingia madarakani.
Amefafanua kwamba, suala la serikali kujiendesha kwa kutegemea mapato yake ya ndani ni kujidanganya kwa kuwa, mlolongo wake unaonesha kuwa makusanyo ya mapato yake yamekuwa yakishuka kila mwezi.
“…kwa mfano wakati Rais Magufuli anaingia madarakani alitegeme mapato ya ndani yatakuwa Sh. 1.6 trilioni kwa mwezi, kwa kiwango hicho serikali ingeweza kukusanya Sh. 19 trilioni kwa mwaka.
“Lakini Februali yalishuka mpaka kuwa trilioni 1.4, Machi trilioni 1.2 trilioni na mwezi Aprili yalishuka tena na kuwa trilioni 1.1. Taarifa zilizopo kutoka mashirika ya fedha na mashirika mengine ya hiyari zinaeleza kwamba, mapato ya serikali hayawezi kuzidi Sh. 12 trilioni kwa mwaka.
Serikali imeingia kwenye mvutano na nchi wahisani ikiwemo uamuzi wa bodi ya taasisi ya Changamoto ya Milenia (Millennium Challenge Corporation) ya Marekani na kufikia hatua ya kusitisha misaada yake kutokana na mambo mawili makuu;
Mosi; Kuvurugwa kwa demokrasia hususani uamuzi wa serikali kurudia uchaguzi wa Zanzibar Machi 20 mwaka huu ambapo ilidaiwa kuwa, chama cha upinzani – Chama cha Wananchi (CUF) kilishinda uchaguzi huo na kupokwa na chama tawala-Chama Cha Mapinduzi (CCM). Uchaguzi huo ulilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na nchi wahisani, ikiwa ni pamoja na Marekani.
Pili; Uamuzi wa serikali ya Tanzania kupitisha Sheria Uhalifu wa Mtandaoni (Cybercrime Act) ya mwaka 2015 licha ya upinzani mkali dhidi ya muswada wa sheria hiyo, iliyotafsiriwa kuwa imelenga kukandamiza uhuru wa habari na haki za binadamu.
Kutokana na hali hiyo Kubenea amesema, hii operesheni ya wafadhili kuzuia misaada itaathiri kwa kaisi kikubwa bajeti ya serikali mwaka huu na kwamba, “kwa sababu mapato yetu ya ndani hawawezi yakatosheleza mahitaji ya serikali.”
Amesema, kwa kuchukua taarifa ya uwezo wa serikali kukusanya Sh. 12 trilioni kwa mwaka, mishahara pekee inagharimu Sh. 6 trilioni kwa mwaka na madeni ya nje yanagharimu Sh. 9.6 trilioni kwa mwaka.
“Hii maana yake tumeishazidi kiasi tunachokusanya kwa mwaka, kwa hiyo serikali italazimika kukopa kutoka kwenye mabenki ya nje ili kujiendesha na hili sio kitu kizuri. Katika nchi 14 wahisani, nchi nane zimejiondoa na sita zimeeleza kufadhili miradi kama kuchimba kisima zenyewe…,” amesema.
Amesema kwamba, miongoni mwa mambo yanayoweza kusaidia nchi ni pamoja na serikali kuangalia namna ya kutatua vikwazo vilivyowekwa ili nchi iende mbele.
“Vikwazo vilivyowekwa na wafadhili vitatuliwe, ili tuweze kupata misaada lazima serikali ivitekeleze. Nchi yoyote rais wake anapoingia madarakani kwa kipindi cha kwanza, huanza kutafuta nchi rafiki mpaka atakaposimama.
“Kwa hiyo rais lazima azunguke duniani aende akatafute wahisani na fedha ili tuendeshe nchi, fedha za ndani ni kama kipaumbele lakini asilimia 20, 30 lazima zitoke kwa nchi wahisani,” amesema.
Post a Comment