Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewakumbusha watumishi wa umma kote
nchini kwamba yeyote atakayeharibu kazi atafukuzwa hapohapo alipo na
hakutakuwa na uhamisho kama ilivyokuwa imezoeleka katika awamu nne za
kwanza za serikali.
Wakati akiwa katika kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25
mwaka jana, mgombea wa CCM wakati huo, Rais John Magufuli alisema
akichaguliwa kuishi katika Ikulu ya Magogoni, hakutakuwa na uhamisho wa
watumishi walioboronga kama ilivyokuwa imezoeleka.
Majaliwa alikumbushia onyo hilo wakati akizungumza na watumishi wa
Wilaya ya Itilima kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo, ambao aliuzindua
jana, mkoani Simiyu.
Alisema watumishi wa umma wako huru kuhamia kokote wapendako lakini
wahakikishe wanaenda huko wakiwa safi na kamwe mtu asiharibu kazi
akitarajia kuwa atahamishiwa sehemu nyingine.
Tangu aingie madarakani Novemba 5 mwaka jana, Rais Magufuli ameshatengua
uhamisho wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Babati, Mussa Natty na
kumrudisha Dar es Salaam.
Kabla ya kuhamishiwa Babati, Natty alikuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Natty alitenguliwa nafasi yake ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Babati
ili arudi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na kusubiri
uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Tuhuma zinazomkabili Natty ni pamoja na usimamizi mbaya uliosababisha
barabara za Manispaa ya Kinondoni kujengwa chini ya kiwango, na
kutochukua hatua kwa watendaji wa manispaa waliokuwa chini yake.
Tuhuma nyingine zinazomkabili Natty ni ukosefu wa uadilifu katika
ubinafsishaji wa eneo la ufukwe wa bahari wa Coco Beach, na malalamiko
ya wananchi juu ya viwanja katika eneo la Kinondoni, ulioambatana na
usimamizi duni wa watumishi hasa sekta ya mipango miji na ardhi.
Akizungumza jana, Majaliwa alisema "serikali hii haina utumishi kwa mtu
aliyeharibu kazi… usije ukaharibu hapa Itilima ukadhani utaenda Bunda
kuendelea na kazi.
"Serikali ya awamu hii haina nafasi na watumishi wa aina hiyo."
Ni wakati wa watumishi kubadilika na kuona mwelekeo wa serikali hii ya
awamu ya tano ukoje, alisema Majaliwa ambaye alisisitiza "jukumu letu ni
kuwatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi zao, rangi wala dini
zao."
Waziri Mkuu aliwahakikishia watumishi hao kwamba Serikali inatambua
changamoto walizonazo kutokana na upya wa wilaya hiyo na mkoa huo na
akawaahidi kuwa itaboresha mazingira yao.
"Msiwaadhibu wananchi kwa kisingizio cha mazingira magumu ya kazi zenu,
tunajua mnayo madai ya nauli, posho za mafunzo, kupandishwa madaraja na
malimbikizo ya likizo."
Alisema serikali itayalipa madeni hayo walau kwa asilimia 80.
Awali, akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Georgina
Bundala alisema ilianzishwa Machi 2012 na kupata Halmashauri Julai 2013,
lakini haina kituo cha polisi cha Wilaya, haina Gereza, Ofisi za
TAKUKURU, mahakama ya wilaya wala benki.
Alisema wilaya hiyo haina hospitali ya Wilaya, lakini imeshatenga eneo la ekari 30 kwa ajili ya ujenzi huo.
"Pia tumeshapima viwanja 123 na eneo la kujenga taasisi lenye ekari 143.8 limefanyiwa thamini na fidia kukamilika," alisema.
Post a Comment