Ufisadi ulioibuliwa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
kwenye bandari ya Tanga, bado unaitesa Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA), ambayo imetoa taarifa ndefu ya kujitetea huku ikikiri kwamba
matishari hayo hayajafanya kazi tangu yanunuliwe.
Matishari hayo yaliyonunuliwa kwa Dola za Marekani 10,113,000 sawa na
zaidi ya Sh. bilioni 21, hayajafanya kazi kwa miaka mitano licha ya
kwamba muuzaji ameshalipwa asilimia 87 ya malipo yake.
Mamlaka hiyo imetoa taarifa kuelezea mchakato mzima wa ununuzi
ulivyoanza mwaka 2011 hadi matishari hayo kufika katika bandari ya
Tanga.
Kwa mujibu wa tarifa ya TPA, matishari hayo kwa mujibu wa mkataba wao na
muuzaji yalipaswa kusafirishwa kwa njia ya kubebwa na meli lakini
haikuwa hivyo.
Ilisema matishari hayo yalivutwa kutumia boti badala ya kubebwa na meli
kama walivyokubaliana kwa madai kuwa matishari hayo yalikuwa makubwa mno
kupakiwa kwenye meli.
Ilisema wakati yakiwa njiani kuja nchini, yalikumbana na dhoruba ya
kimbunga kikali baharini na kusababisha boti iliyokuwa ikiyavuta kuzama
na matishari hayo kugongana kisha kusukumwa na mawimbi hadi nchini
Malaysia.
TPA ilisema ajali hiyo ilisababisha matishari hayo kupata hitilafu
lakini kwasababu yalikuwa na bima, gharama za matengenezo zilibebwa na
bima iliyokuwa imekatwa.
Ilisema baada ya matengenezo yalivutwa hadi bandari ya Tanga na
yalipofanyiwa ukaguzi yalibainika kuwa na kasoro kadhaa zilizosababisha
zisifanye kazi iliyokusudiwa kwa wakati huo.
“Yalikuwa na mifuniko ambayo ilibainika kuwa si rafiki katika shughuli
za kupakia na kupakua na muuzaji alitakiwa kuyafanyia matengenezo kwa
gharama zake mwenyewe,” ilisema taarifa ya TPA.
Aidha, TPA ilifafanua kuwa wakati matishari hayo yakifanyiwa majaribio
kulikuwa na changamoto kadha kama vile ukubwa wa tishari kusababisha
kreni za meli kushindwa kupanga mizigo vizuri.
Ilisema kulihitajika boti kubwa kwa ajili ya kuvuta matishari hayo na
kwamba tayari mamlaka imeiagiza na inatarajiwa kufika nchini kuanzia
Juni.
Mamlaka hiyo ilisema imemwagiza muuzaji wa matishari hayo kuyafanyia
marekebisho na kuhakikisha yanakuwa katika hali ya kutumika na ndipo
atakapolipwa malipo yake ya mwisho.
TPA ilisema kwenye taarifa yake kuwa bado inadaiwa Dola za Marekani
milioni 1.4 (sawa na zaidi ya Sh. bilioni 3) tu na muuzaji huyo.
Malaka hiyo imesema zitalipwa baada ya majaribio kufanyika na kubainika kuwa matishari hayo yanaweza kufanya kazi iliyokusudiwa.
Mamlaka hiyo ilitoa zabuni ya kutengenezewa matishari matatu kwa mtu
aitwaye John Achelis na kampuni ya Sohne Gmbh ambapo kila moja lilipaswa
kuwa na ukubwa wa tani 3,500.
Post a Comment