Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo, amempa wiki tatu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngulumi, kuhakikisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato na uendeshaji wa soko la Ilala unakuwa sawa.
Jafo alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam, alipotembelea
wafanyabiashara wa soko hilo na kuzungumza nao kuhusu kero
zinazowakabili.
Alisema wafanyabishara hao walimlalamikia kutozwa ushuru wa Sh.300 ya
Manispaa na Sh.400 ya vyama vya ushirika kila siku, ambazo zinaliwa na
wajanja huku vizimba vya mama lishe vikimilikiwa na madalali wa soko
badala ya wafanyabiashara.
“Mkurugenzi nitarudi hapa baada ya wiki tatu nikute huu mfumo wa
ukusanyaji wa kodi za kero kwa wafanyabiashara ambazo zinaingia kwenye
mifuko ya wanjanja umesharekebishwa,” alisema Jafo.
“Soko ni chafu, matatizo ni mengi, wanaofaidika katika soko hili ni wajanja wanja na siyo wafanyabishara.
"Mkurugenzi hakikisha unakaa na wafanyabishara wote ambao wako kwenye
soko hili ili wakueleze matatizo yaliyopo na nikirudi hapa nikute haya
matatizo mmeyamaliza.”
Jafo ambaye alitembezwa katika maeneo yote ya soko, alishuhudia maji
taka yakitiririka kwenye biashara na kuiagiza halmashauri hiyo
irekebishe chemba za vyoo haraka iwezekanavyo ili kuepusha kuzuka kwa
ugonjwa wa kipindupindu.
Awali, wafanyabishara wa soko hilo walimlalamikia Jafo kuwa ushuru ambao
wamekuwa wakitozwa unaingia kwenye mifuko ya watu binafsi huku wabeba
mizigo nao wakitozwa ushuru ingawa hawana eneo la bishara.
Katibu wa mama lishe katika soko hilo, Janeth Nyanda, alisema vizimba
vya mama lishe vinamilikiwa na wapangaji ambao wamevipangisha kwa
Sh.80,000 hadi 100,000 kwa mwezi huku wakiilipa halmashauri Sh. 9,000 tu
kwa mwezi.
Naye Japheth Magira, mfanyabishara wa nazi, alimlalamikia Jafo kuwa
wamkuwa wakitozwa ushuru wa kupaki magari la kushusha mzigo wa Sh.30,000
kwa siku, na tofauti na fedha za ushuru.
Akijibu sababu za ukusanyaji wa mapato holela katika soko hilo,
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mngurumi, alisema wanaoshiriki kukusanya
Sh.400 ni wafanyabishara wenyewe ambao wamejiunga na vyama vyao vya
ushirika.
Kuhusu mapato ya soko alisema wanakusanya Sh. milioni 35 kwa mwezi baada ya kuondoa gharama za usafi.
“Naahidi kushughulia maagizo yote niliyoagizwa na Naibu Waziri na tuko
kwenye mpango wa kuboresha masoko haya yote ya Manispaa hii,” alisema
Mngurumi.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment