1.1. Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania ni taasisi ya Serikali yenye dhamana ya
kusimamia shughuli za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta hapa nchini.
Kuwepo kwa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya
2010 na Kanuni za EPOCA (CEIR) za mwaka 2011 zimewezesha kutekelezwa kwa
mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya
mkononi.
1.2. Mfumo
huu wa kielektroniki ulizinduliwa rasmi tarehe 17 Desemba 2015 na
unahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya
mkononi (IMEI) kwa lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa
vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango (bandia)
vya matumizi katika soko la mawasiliano. Namba tambulishi za vifaa vyote
vya mawasiliano vya mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au
visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano
havitaruhusiwa kuunganishwa kwenye mitandao ya watoa huduma ifikapo
kesho tarehe 16 Juni 2016.
1.3. Kipindi
cha mpito cha kuelimisha umma pamoja na zoezi la wateja kuhakiki simu
walizo nazo au wakati wanataka kununua simu mpya lilianza mwezi Desemba
2015 wakati mfumo ulipozinduliwa na litamalizika kesho tarehe 16 Juni
2016. Hata hivyo, elimu kwa umma kuhusu simu bandia imekuwa ikitolewa
nchini tangu mwezi Novemba 2011 baada ya Kanuni za CEIR kutoka, kufuatia
kupitishwa na Bunge Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta
tarehe 20 Juni 2010 ikielekeza kuwekwa kwa mfumo wa namba za utambulisho
wa vifaa vya Mawasiliano vya kiganjani.
2.0 KAZI ZILIZOFANYIKA TANGU KUZINDULIWA KWA MFUMO
2.1
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeendelea kusimamia kwa karibu
makampuni ya simu hapa nchini katika uendeshaji wa kila siku wa mfumo wa
rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi.
Hii imesaidia pamoja na mambo mengine kupata taarifa za namba tambulishi
(IMEI) na kuzifanyia uchambuzi wa kina ili kupata mwelekeo halisi kabla
ya kipindi cha mpito kuisha hapo tarehe 16 Juni, 2016.
2.2
Mamlaka ya Mawasiliano iliendelea pia na kampeni za kutoa elimu kwa
umma kuhusu jinsi ya kuhakiki namba tambulishi (IMEI) za vifaa vya
mkononi (mobile devices). Katika kampeni hizo wananchi walipata uelewa
wa kutambua uhalisia wa simu zao ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya
kuzingatia wakati wa kununua simu mpya. Makampuni yote ya simu hapa
nchini kwa nyakati tofauti wameshiriki pia katika kuelimisha umma, ikiwa
ni pamoja na kuwapelekea ujumbe mahususi moja kwa moja kwa watumiaji
wote wa simu za mkononi. Hali kadhalika Shirika la Viwango Tanzania na
Tume ya Ushindani nchini, wameshiriki moja kwa moja katika kutoa elimu
kwa umma sambamba na Mamlaka ya Mawasiliano.
2.3
Kipindi cha kuanzia Desemba 2015 mpaka mwezi Mei 2016 Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania ilitoa elimu kwa umma katika mikoa ya Tanga,
Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Iringa, Dodoma,
Singida, Tabora, Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na Kagera. Pia
elimu kwa umma ilitolewa Zanzibar. Mamlaka imefanya pia elimu kwa umma
katika miji ya, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara wiki iliyopita pamoja
na wiki hii. Aidha kesho ambayo ndio siku ya ukomo wa matumizi ya simu
bandia nchini, kutakua na mkutano wa wafanya biashara wa simu wa mkoa wa
Dar es Salaam. Mkutano huo utawahusisha pia mafundi wa simu, Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya mkoa. Pamoja na mikutano ya hadhara na mikutano ya
barabarani (road shows), elimu imetolewa kwa wauzaji wa simu, Mafundi wa
Simu na Maafisa Biashara pamoja na Kamati za Ulinzi na Usalama za
maeneo husika.
3.0 UCHAMBUZI WA NAMBA TAMBULISHI (IMEI)
Wakati mfumo wa rajisi
ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi
unazinduliwa mwezi Desemba 2015, idadi ya namba tambulishi ambazo
zilikuwa hazina viwango (bandia) zilikuwa sawa na 4% na zile ambazo
zilikuwa zimenakiliwa (duplicates) zilikuwa ni sawa na 30%. Hii ikiwa na
maana 66% ni sio simu bandia. Uchambuzi huu haukuhusisha taarifa za
makampuni ya Viettel na Smile.
Kielelezo 1: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Disemba, 2015
Uchambuzi
wa mwezi Februari 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo
zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na 3%, vilevile idadi ya namba
tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na 18%. Simu halisi
zilikuwa sawa na 79%.
Kielelezo 2. Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI)February 2016
Uchambuzi
wa mwezi Machi 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo
zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na 4%, na idadi ya namba
tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na 13%. 83% zikiwa simu
halisi. Uchambuzi huu unahusisha taarifa za makampuni yote ya simu
nchini.
Kielelezo 3: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Machi, 2016
Uchambuzi
wa mwezi Aprili 2016 unaonyesha hakuna mabadiliko yoyote ya idadi ya
namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (invalid) hivyo kubakia
4%, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa ziliongezeka kutoka
13% na kufikia 14%. Vilevile idadi ya namba tambulishi za simu halisia
ilipungua kutoka 83% mpaka 82% kama ilivyoonyeshwa katika kielelezo
kifuatacho.
Kielelezo 4: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Aprili, 2016
Matokeo
ya uchambuzi wa mwezi Aprili, 2016 umeonyesha namba tambulishi ambazo
zilikua zimenakiliwa kuongezeka na kuleta taswira kuwa kuna uwezekano
mkubwa kwa wauzaji wa simu wasio waaminifu kupunguza bei za simu zao
zenye namba tambulishi zilizonakiliwa na kuwafanya watumiaji wa simu
katika maeneo husika ambayo elimu kwa umma ilikua bado haijawafikia
kushawishika kununua simu hizo. Matokeo
haya yalitoa msukumo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania pamoja na
wadau wote kuongeza nguvu zaidi kuelimisha wananchi katika maeneo
yaliyobakia kuhusu umuhimu wa kuhakiki simu zao ikiwa ni pamoja na
kuelewa zaidi utaratibu wa kufuata wakati mtu atakapo hitaji kununua
simu mpya.
Kielelezo 5: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Mei, 2016
Uchambuzi
wa mwezi Mei, 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa
hazina viwango zilikuwa sawa na 3%, na idadi ya namba tambulishi ambazo
zimenakiliwa zilikuwa sawa na 2% ambapo 95% zikiwa simu halisi.
Uchambuzi huu unahusisha taarifa za makampuni yote ya simu nchini.
Matokeo
haya mazuri yanaonyesha matokeo ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Makampuni ya simu hapa nchini pamoja na
wadau wengine katika kuelimisha umma juu ya kuhakiki uhalisia wa simu
walizo nazo ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa
kununua simu mpya.
Kielelezo 6: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Juni, 2016
Uchambuzi
uliofanywa tarehe 14 Juni 2016 unaonyesha mabadiliko chanya ya idadi ya
namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (invalid) kupungua
kutoka 3% hadi kufikia 2.96%, na idadi ya namba tambulishi ambazo
zimenakiliwa zikipungua kutoka 2% hadi kufikia 0.09%. Vilevile idadi ya
namba tambulishi za simu halisia zimeongezeka kutoka 85% mpaka 96.95%
kama ilivyoonyeshwa katika kielelezo 6 hapo juu.
Matokea
haya yanaonyesha mwitikio mzuri wa wananchi juu ya uelewa wao katika
suala zima la uzimaji wa simu ambazo hazikidhi viwango. Matokeo hayo
yanatoa picha nzuri hasa tunapoelekea kuhitimisha zoezi la uzimaji wa
simu bandia kesho tarehe 16 Juni 2016.
4.0 CHANGAMOTO
Pamoja
na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Mamlaka pamoja na wadau wengine
bado kuna changamoto ambazo zinahitajika kutatuliwa. Changamoto hizo ni
pamoja na:
(i) Uaminifu mdogo kwa baadhi waauzaji wa simu kwa kutoa punguzo kwa wananchi ili kuwashawishi kuzinunua simu bandia kwa bei nafuu;
(ii) Gharama
zinazohitajika katika kuwafikia wananchi na kuelimisha ili waweze
kuelewa zaidi juu ya mpango mzima wa kuhakiki simu zao; na
(iii) Uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi katika kuitikia wito wa kuhakiki simu zao katika kipindi cha mpito.
5.0 HITIMISHO
Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania inaendelea kumbusha watanzania wote kuwa ni
jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa simu yake ni halisi na sio
bandia kwani kuanzia kesho, hakuna simu bandia itakayoweza kufanya kazi
nchini. Vilevile Mamlaka inawakumbusha wauzaji wa vifaa vya mawasiliano
vya mkononi kutambua kuwa ni kosa kubadilisha namba tambulishi za vifaa
vya simu za mkononi (mobile devices) kwani adhabu yake ni kifungo
kisichozidi miaka kumi (10) au faini isiyopungua TZS millioni 30 au
vyote kwa pamoja.
Mamlaka
inatoa wito kwa wale wote wote wanaofanya biashara za kuingingiza simu
hapa nchini kutoka nje wahakikishe kuwa simu wanazoleta zinakidhi
viwango, zimehakikiwa kwa mujibu wa Shirika la Viwango Tanzania. Aidha
Mamlaka inawakumbusha kwa mara nyingine kuwa wanapaswa kuwa na leseni ya
Mamlaka ya Mawasiliano kwa mujibu wa Sheria. Hii pia ni kwa mafundi
wote wa simu nchini, wanatakiwa kuanza mchakato wa kupata leseni ya
kutengeneza simu, ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuwaorodhesha
wanaoleta simu zao kutengenezwa ili kuepuka kuwa sehemu ya mtandao wa
wizi wa simu.
Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania inayapongeza makampuni ya simu kwa ushirikiano
mzuri wanaondelea kuuonesha katika kutekeleza agizo hili la Serikali
kupitia Mamlaka. Hali kadhalika, jitihada zao za kushiriki elimu kwa
umma kwa wateja wao pamoja na kuwapatia simu wateja waliokuwa wanatumia
simu bandia, kumepelekea agizo hili kufanikiwa kwa kiwango cha hali ya
juu. Mafanikio ya jambo hili, kwa kiasi kikubwa yametokana na
ushirikiano wa wadau mbalimbali wa Mawasiliano, wakiwemo jeshi la
Polisi, Tume ya Ushindani pamoja na Shirika la Viwango Tanzania.
Mhandisi James Kilaba
KAIMU MKURUGENZI MKUU
15 Juni, 2016
Maelezo ya ziada kwa Wahariri
FAIDA ZA MFUMO WA RAJISI YA NAMBA TAMBULISHI
Mfumo huu wa rajisi una faida zifuatazo:
- Kuthibiti wizi wa simu. Iwapo mtu atapoteza au ameibiwa simu ya kiganjani na akatoa taarifa kwa mtoa huduma, simu hiyo itafungiwa isiweze kutumika kwenye mtandao mwingine wowote wa simu za kiganjani. Mteja anaponunua simu ni lazima adai risiti halali na halisi na pia garantiii ya miezi 12. Mteja anatakiwa aihifadhi risiti hiyo angalau kwa miezi mitatu. Baada ya hapo, iwapo simu imekuwa inatumika, taarifa za matumizi zinaweza kutumika kama uthibitisho mbadala wa milki ya simu husika.
- Kuhimiza utii wa sheria: Kifungu cha 128 cha EPOCA kinamtaka mtumiaji wa simu kutoa taarifa ya kupotea au kuibiwa kwa simu au laini ya simu. Kifungu cha 134 kinayataka makampuni ya simu kutokutoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa kama ilivyoelezwa hapo juu. Mara tu mteja anapopoteza simu yake ya kiganjani anatakiwa kutoa taarifa kwa kituo cha Polisi cha karibu ambapo atapewa namba ya kumbukumbu ya taarifa ya tukio, maarufu kama RB. Anatakiwa aende kwa mtoa huduma kutoa taarifa ya tukio akiwa na hiyo RB na uthibitisho wa umilki wa simu iliyopotea (risiti aliyopewa wakati wa kununua iwapo itakuwepo).
Mtoa
huduma kwanza atahakiki umilki wa simu iliyopotea au kuibiwa na
atampatia mteja namba ya kumbukumbu kwamba simu hiyo imefungiwa
isutumike kwenye mitandao ya simu na hatimaye ataifungia simu hiyo ndani
ya saa 24.
- Kujenga misingi ya matumizi ya simu halisi, zisizo bandia. Mtumiaji ataweza kutambua iwapo simu aliyo nayo inakidhi viwango, ni halisi na sio bandia.
Post a Comment