Ukatili uliofanywa na watu wasiojulikana wa kuwachinja watu wanane wa
kitongoji cha Kibatini mkoani Tanga, umesababisha wakazi wa kitongoji
hicho kuanza kuyahama makazi yao.
Watu hao walichinjwa usiku wa
Mei 31 nje ya nyumba ya mwenyekiti wa kitongoji hicho kwa madai kuwa
walisababisha “vijana” wao kukamatwa na polisi baada ya kutoa taarifa
zao wakati wakizurura kwenye eneo lao.
Waliouawa katika tukio
hilo ni mwenyekiti huyo, Issa Hussein, kaka yake, Mkola Hussein, Hamis
Issa, Issa Ramadhani na wengine wawili waliotambulika kwa jina moja la
Kadir, Mikidadi na Salum.
Jana baada ya mazishi ya watu hao,
mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk alipeleka lori aina ya Mitsubishi
Fusso kwa ajili ya kuwahamisha wanakijiji hao.
Wakazi wayahama makazi
Diwani wa kata ya Mzizima, Fredrick Chiluba alisema wakazi wa Kibatini
wameamua kuhamia kitongoji cha Kona-Z kilichopo kijiji jirani Kiomoni.
Mwandishi alishuhudia wakazi takriban 60 wa Kibatini wakitoa vyombo, huku wengine
wakiezua mabati kwenye nyumba zao wakati wakisubiri gari ambalo baadaye
liliwasili na kuwachukua.
“Wameingiwa na hofu ya kibinadamu na
jambo hili lipo moyoni mwa mtu, hivyo huwezi kumng’ang’aniza kukaa hapo
wakati anahisi hayupo salama,” alisema Chiluba.
Hadija Hussein
alisema wameamua kuhama kwa sababu mara baada ya kukamilishwa kwa
shughuli za mazishi ya ndugu zao wanne, ilipofika saa 6:00 usiku, askari
waliokuwepo kwenye viwanja vya nyumba ya marehemu Mkola Hussein kulinda
usalama hawakuonekana.
“Tulipatwa
na wasiwasi mkubwa tulipoona askari na magari yao wameondoka, tukajua
sasa na sisi tunakuja kuchinjwa.Hatukupata usingizi kwa hofu, ndipo
asubuhi tukaamua kuondoa vyombo,” alisema.
Alisema mbunge alipokwenda kuwahani, walimuomba gari la kuhamisha vyombo vyao ili waondoke kabla jioni haijafika.
Mbunge
Mbarouk alisema alipowasili eneo hilo na kukuta hakuna ulinzi,
alimpigia simu mkuu wa polisi wa Wilaya ya Tanga ambaye alipeleka
askari.
“Nilipowauliza viongozi wa Jeshi la Polisi waliniambia
askari wapo wanafanya kazi ya kuzungukia maeneo, lakini haikuwa haki
kuwaondoa askari mara tu baada ya kufanyika mazishi,” alisema Mbarouk.
Mbunge
huyo alisema ameushauri uongozi wa polisi kupeleka ulinzi hata
wanakohamia kwa sababu wauaji lazima watapata taarifa ya waliko na
wanaweza kuwatendea chochote.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,
Leonard Paulo alisema askari hawakuwa wameondoka kijijini hapo bali
walikuwa wamefanya mbinu za kufanya doria maeneo yanayozunguka kitongoji
hicho.
“Usiku huo kwenye kitongoji kulikuwa na kikosi maalumu
cha FFU ambacho mimi mwenyewe nilikuwa nakiongoza usiku kucha. Tulikuwa
tukifuatilia maficho ya wahalifu, kitaalamu tunaita undercover,”
alisema.
Kamanda huyo alisema wakati polisi ikiendelea na operesheni, si
vyema kuwatisha wananchi kwa kuwa tangu yalipofanyika mauaji hayo,
askari hawajaondoka.
RC: Mauaji ya Tanga si ugaidi
Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, Martine Shigela amesema mauaji yanayotokea katika mitaa ya jijini
Tanga na Amboni si vitendo vya kigaidi, bali yanatendwa na kundi la
watu wanaotaka kuvuruga amani.
Amesema hii ni vita ya kiuchumi
inahusiana na ujio wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga na
kwamba Serikali itahakikisha inawakamata waliohusika.
Alisema
hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa Serikali, Halmashauri ya
Wilaya ya Muheza pamoja na vyama vya siasa vya wa wilayani humo.
Shigela,
ambaye alikuwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza kupokea taarifa
ya maendeleo ya kabla ya kuanza ziara wilayani humo, alisema Serikali
haiwezi kukubali kuona kundi la watu wachache wanaharibu amani iliyopo.
Post a Comment