Rais Dk. John Magufuli, amemrudisha nyumbani aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, pamoja na watumishi wengine watano, baada ya muda wao kumalizika.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Dk. Magufuli kuwarejesha nyumbani Mabalozi
wa Tanzania walioko nchi za nje baada ya muda wao wa mkataba kumalizika.
Ikumbukwe kuwa Januari 25, mwaka huu, Rais Magufuli alimrejesha nyumbani
Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Peter Kallaghe, kuja
kufanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kikanda na Kimataifa, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Dk.
James Msekela na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan, Dk. Batilda
Buriani, baada ya mikataba yao kumalizika.
Akizungumza na Nipashe, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, alisema
kurudhishwa nyumbani kwa Balozi Msuya, ni jambo la kawaida kwa sababu
bado kazi ya kuwarudisha nyumbani Mabalozi waliomaliza mikataba yao
linaendelea.
Alisema kwa sasa serikali inachofanya ni kuwarudisha nyumbani Mabalozi
ambao mikataba yao imemalizika na kuwapeleka watumishi wengine wakapate
uzoefu nje ya nchi.
Alisema kuna makundi matatu ambapo kundi la kwanza ni watumishi wa idara
ambao muda wao wa miaka mitano umemalizika ambao wanarudishwa nyumbani
ama kuhamishiwa kituo kingine cha kazi.
Alisema kundi la pili ni la Mabalozi ambao siyo watumishi wa wizara,
lakini waliteuliwa na Rais kwa mkataba, hivyo mikataba yao ikimalizika
Rais mwenyewe ndiye anayeamua kama ni kuwaongezea au kusitisha na kurudi
nyumbani.
Dk. Mahiga alitaja kundi la tatu kuwa ni Mabalozi ambao muda wao wa
kukaa nje umemalizika au umri wao wa kustaafu umefika, lakini mikataba
yao bado haijamalizika, hivyo Rais anaamua kuwarudisha nchini ili
wapumzike na wengine wakashike nafasi zao.
Alisema kuna Mabalozi ambao mikataba yao ya kufanya kazi nje ya nchi ni
miaka mitano, lakini wamekaa zaidi ya miaka 10, hivyo serikali iko
katika mchakato wa kuwarudisha nyumbani.
Waziri Mahiga alisema kuna vituo zaidi ya 35 ambavyo vinatakiwa kuwa na
Mabalozi, hivyo serikali itahakikisha inawarudisha nyumbani mabalozi
waliomaliza muda wao wa kazi na kupangiwa majukumu mengine.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment