Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla amezindua mradi wa kutokomeza vifo vya wajawazito na watoto wachanga nchini katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.
Mradi huo unaofadhiliwa na taasisi ya Vodacom Foundation kwa
kushirikiana na mashirika ya kimataifa ya Usaid, Path Finder na Touch
Foundation, ulizinduliwa jana.
Mradi huo unaojulikana kama `Moyo' awamu ya pili, umelenga kuunga mkono
jitihada za serikali za kuboresha sekta ya afya nchini na adhma ya
kutokomeza vifo vya wajawazito na watoto wachanga nchini.
Dk. Kigwangalla alisema mradi huo unakwenda sambamba na malengo ya
serikali ambayo imejipanga kuhakikisha matukio ya vifo vya wajawazito na
watoto wachanga vinavyojitokeza wakati wa kujifungua kutokana na
ukosefu wa huduma za matibabu. vinatokomezwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao, alisema tangu mradi
wa Moyo awamu ya kwanza uanze kutekelezwa mwaka 2009, umeandikisha
wanawake zaidi ya 16,000 katika vituo vya afya na kuokoa maisha ya
wajawazito na watoto zaidi ya 450.
Alisema zipo changamoto kadhaa za baadhi ya wajawazito kutojifungua
katika vituo vya afya, ambapo licha ya changamoto hizo mradi huo
umewezesha mafunzo kwa wahudumu wa afya wa ngazi ya jamii wanaopita kila
kaya kutoa elimu ili kubadili mitazamo hasi ya baadhi ya akina mama
kutofika kwenye vituo vya afya kupatiwa huduma za uzazi.
“Kupitia mradi huu ambao pia umelenga kurejesha fadhila kwa wateja wetu,
tutagharimia usafiri wa wajawazito kupitia huduma ya M-Pesa kama
ambavyo ilikuwa kwenye awamu ya kwanza ya mradi ili waende kwenye vituo
vya afya kupata matibabu haraka pindi patakapohitajika msaada," alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Vodacom Foundation, Balozi
Mwanaidi Sinare Maajar, alisema pamoja na mafanikio ya kiafya
yaliyopatikana kwa kukabiliana na ugonjwa wa fistula na huduma ya ujumbe
mfupi wa maneno ya kuelimisha akina mama masuala ya uzazi kupitia mradi
wa `Wazazi Nipendeni' kusaidia akina mama wengi, vile vile shughuli
hiyo imekuwa ikiviwezesha vikundi vya kuweka na kukopa vya wanawake na
kuwapatia mafunzo ya kuwawezesha kijikwamua kiuchumi.
Mkazi wa Sengerema, Lawrencia John, ambaye ni mmoja wa wanawake
walionufaika, aliupongeza mradi huo akisema ulimsaidia alipokuwa
anajifungua mtoto wake wa kwanza.
"Nilipopiga simu, nilisaidiwa mara moja na nikajifungua salama kabisa na
natoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kunufaika na huduma hii,"
alisema.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment