WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itamchukua hatua kiongozi yeyote
atakayedonoa fedha za michango ya madawati inayotolewa na wadau
mbalimbali wa maendeleo.
Pia
amewaagiza watendaji wote wa Serikali, Walimu Wakuu wa Shule za Msingi
na Sekondari, Maofisa Elimu, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya
na Wakuu wa Mikoa, kuhakikisha michango hiyo inayotolewa inawafikia
walengwa.
Aidha,
amezitaka wilaya zote nchini zianzishe mpango endelevu wa kuhakikisha
kwamba upungufu wa madawati unasahaulika kabisa katika maeneo yao na
kwamba utendaji wa viongozi wa elimu na Serikali katika ngazi mbalimbali
utapimwa kutokana na jinsi ambavyo wametekeleza maagizo hayo.
Waziri
Mkuu Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Juni 11, 2016) wakati wa
matembezi ya hisani ya kukusanya fedha za kununulia madawati kama sehemu
ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania
(BOT).
Katika
maadhimisho hayo yaliyoanzia BOT hadi viwanjja vya Mnazi Mmoja, Gavana
wa BOT, Profesa Benno Ndulu alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya shilingi
milioni 263 zilizochangwa na benki hiyo pamoja na watumishi wake kama
mchango wao kwa ajili ya ununuzi wa madawati.
Waziri
Mkuu aliwapongeza watumishi wa BOT kwa kushirikiana na Serikali katika
kutatua changamoto hiyo ambapo alitoa wito kwa taasisi zote katika sekta
ya umma na binafsi pamoja na watu binafsi kuchangia uboreshaji wa elimu
nchini kama sehemu ya “Majukumu ya Taasisi kwa Jamii” (Corporate Social
Responsibility).
Amesema
kuwa na elimu bora, siyo tu faida kwa Taifa, bali kwa waajiri pia,
kwani itahakikisha kwamba taasisi za umma na binafsi zinapata
wafanyakazi ambao wameiva na wenye weledi wa kutekeleza majukumu
mbalimbali ya uzalishaji katika taasisi hizo.
“Nitoe
wito pia kwa wanafunzi wote ambao watafaidika na kuboreshwa kwa
mazingira ya kusomea, ikiwemo kupewa madawati na mahitaji mengine,
kuhakikisha wanasoma kwa bidii kwa faida yao na Taifa kwa ujumla na kwa
kufanya hivyo, wanafunzi watakuwa wanaenzi jitihada za Serikali, taasisi
za umma, taasisi binafsi na watu binafsi katika kuboresha elimu
nchini,” amesema.
Amesema
Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kupambana na changamoto za sekta ya
elimu na kwamba tangu Uhuru, Serikali za Awamu zote zimekuwa zikifanya
jitihada mbalimbali katika kuboresha elimu kwa wananchi wake.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU.
Post a Comment