WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali
inaendelea na jitihada za kuondoa tatizo la uhaba wa sukari nchini
ambapo jumla ya tani 20,000 zilisambazwa jana katika maeneo mbalimbali
nchini.
Amesema
shehena nyingine ya tani 35,000 inatarajiwa kusambazwa hivi karibuni
katika kanda zote nchini hivyo amewataka wafanyabiashara watakapoipokea
kuiuza kwa wananchi bila ya kuificha na bei isizidi shilingi 2,200.
Waziri
Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jana jioni ( Ijumaa, Juni 10, 2016) wakati
akizungumza na Masheikh na Viongozi wa Kamati ya Amani ya mkoa wa Dar
es Salaam alipowaalika katika futari aliyoiandaa nyumbani kwake.
Amesema
tayari viwanda vimeanza kufunguliwa na tani 300 zilizotoka katika
kiwanda cha Sukari cha Kagera zitasambazwa katika wilaya za Kakonko,
Kibondo, Kasulu, Uvinza na Kigoma ili kutosheleza maeneo hayo.
Hata
hivyo amewataka Maofisa Biashara katika Halmashauri zote nchini
kuendelea kufanya ufuatiliaji katika maduka ili kuhakikisha bidhaa hiyo
inapatikana na hakuna mfanyabiashara atakayeificha.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara kote nchini
kutopandisha bei za vyakula katika kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu
wa Ramadhani.
Akizungumza
kuhusu tabia za baadhi ya wafanyabiashara wanaopandisha bei za bidhaa
hasa vyakula katika kipindi hiki cha mfungo amewataka kumuogopa Mwenyezi
Mungu kwa sababu kitendo hicho kinawapa wafungaji wakati mgumu.
“Kufunga
Ramadhani si jambo la anasa, si matashi binafsi bali ni jambo la
kiimani hivyo tusipandishe bei ya bidhaa kwa lengo la kuwaadhibu Waislam
kwa sababu tu wamefunga.
“Katika
Quran surat Baqarah aya ya 183 inasema kwamba enyi mlioamin
imefaradhishwa kwenu kufunga kama walivyoamrishwa kufunga kwa waliopita
kabla yenu ili muwe wachamungu, hivyo hatuna budi kufunga” alisisitiza.
Alisema
tabia hiyo si nzuri na imekuwa ikijitokeza mara kwa mara unapofika
wakati wa mfungo kwa wafanyabiashara kuamua kupandisha bei hivyo
aliwataka waiache kwani Serikali haitawavumilia na atakayethubutu hatua
kali zitachukuliwa dhidi yake.
Share:
Post a Comment