Benki
Kuu ya Tanzania (BOT) na wafanyakazi wake wa matawi yote nchini kwa
kushirikana na baadhi ya Taasisi za kifedha na kampuni za simu nchini,
imetoa Shilingi Milioni 273 kuchangia ununuzi wa madawati ikiwa ni
sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Benki hiyo.
Fedha hizo zilikabidhiwa leo kupitia hundi ya mfano kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya matembezi ya hisani yaliyolenga kuchangia madawati, yaliyoanzia Ofisi za BOT hadi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
kabla ya kukabidhi fedha hizo, Gavana wa BOT Prof. Benno Ndulu alisema
lengo la mchango huo ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano
katika kuongeza ubora wa elimu kupitia upatikanaji wa madawati kwa
shule za msingi na sekondari nchini.
“Tunatambua
kwamba changamoto hiyo (uhaba wa madawati) ni kubwa, lakini tunaamini
mchango wetu utasaidia kupunguza makali ya tatizo hilo na kuongeza idadi
ya watoto wetu ambao wanasoma wakiwa wamekaa kwenye madawati” alisema Gavana Prof. Ndulu
Akifafanua
mchango huo, Gavana Prof. Ndulu alisema kati ya fedha hizo, BOT imetoa
Shilingi Milioni 167, Wafanyakazi Milioni 29.8, Taasisi za Kifedha
Milioni 22 na kampuni za simu Milioni 54.3 na kwamba madawati hayo
yatasambazwa kwenye shule zenye upungufu au ukosefu wa madawati za Dar
es Salaam na zilizoko mikoa ambayo Benki hiyo ina matawi yake.
Alitaja
mikoa hiyo na fedha zilizochangwa na wafanyakazi wa BOT wa matawi ya
mikoa hiyo kuwa ni Makao Makuu Dar es Salaam waliochangia Shilingi
Milioni 22, Mwanza (Milioni 1.24), Chuo cha Benki Mwanza (680,000)
Arusha (Milioni 1.23) Mbeya (Milioni 1.186), Mtwara (850,000) na Dodoma
(Milioni 1.18).
Alisema
taasisi zilizochangia fedha hizo ni Benki ya India Shilingi Milioni 5,
Benki ya Habib (Milioni 5), Benki ya Exim (Milioni 5), Benki ya UBA
(United Bank for Africa, Milioni 2), Tanzania Mortgage Refinance
(Milioni 2), China Community Bank (Milioni 2) na NIC Bank aliyotoa
Milioni 1.
Kwa
upande wa kampuni za simu zilizotoa fedha ni kampuni ya Vodacom
iliyotoa Dola za Kimarekani 10,000, kampuni ya Tigo Dola za Kimarekani
10,000 na kampuni ya Selcom iliyotoa Dola za Kimarekani 5,000.
Akizungumza
baada ya kupokea hundi ya mfano, Waziri Mkuu Majaliwa alisisitiza fedha
hizo zitumike kama zilivyokusudiwa na yeyote atakayetumia fedha hizo
kinyume na malengo achukuliwe hatua mara moja.
Katika
kuthamini sekta ya elimu nchini, Gavana Prof. Ndulu alisema benki hiyo
ilianzisha Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambapo
hadi sasa umetoa ufadhili kwa wanafunzi 22 kusoma shahada za kwanza na
za uzamivu katika vyuo vikuu hapa nchini katika masomo ya sayansi,
hisabati, uchumi, fedha, uhasibu na TEHAMA.
“Lengo
kubwa la mfuko huu ni kuhamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya
sayansi na hisabati yakiwemo masomo kuhusu gesi na mafuta.Katika idadi
hiyo, 16 ni wanafunzi wa kike na waliobaki 8 ni wanaume” alisema Gavana Prof. Ndulu.
Benki
Kuu ya Tanzania (BOT) ilianza kutoa huduma kwa wananchi mnamo tarehe 14
Juni mwaka 1966 na Juni 14 mwaka huu inatimiza Miaka 50 na katika
kuadhimisha miaka hiyo wafanyakaz wa matawi yote nchini wanafanya
matembezi hayo ili kutoa mchango kwa jamii.
Post a Comment