Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi na silaha za moto kuwatawanya wananchi hao, ambao nao wanadaiwa kuvunja sheria kwa kuwashambulia askari kwa mawe katika eneo la darajani, Tarakea.
Shughuli za usafirishaji katika eneo hilo (Tarakea) ambalo ni la mpakani mwa Tanzania na Kenya, zilisimama kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni wakati ulipopatikana muafaka, hatua iliyotokana na baadhi ya viongozi kwenda kuzungumza na wananchi.
Ajali hiyo ilisababisha kifo cha mwendesha bodaboda (jina lake halikufahamika mara moja) na ndipo wananchi walipofunga barabara ya Moshi-Tarakea- Nairobi kwa mawe na hivyo kusimamisha shughuli zote za usafirishaji ili kuishinikiza serikali kuiamuru Ofisi ya Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoani Kilimanjaro kuweka matuta katika eneo la Mailisita hadi Bonite ambako kumekuwapo na matukio ya mara kwa mara ya ajali.
Wafanyabiashara wengi wa mikoa ya kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga hupenda kutumia barabara hiyo kutoka Tanzania kwenda jijini Nairobi, Kenya kutokana na ufupi wake kwa sababu hutumia saa 3 hadi 3:30 kusafiri kati ya maeneo hayo.
Mfanyabiashara wa mazao, Andrew Sanika aliiambia Nipashe kwa njia ya simu jana asubuhi kwamba magari yote ya mizigo pamoja na abiria waliokuwa wakitokea eneo la mpakani maarufu kama ‘Custom’, kwa upande wa Kenya kuja Tanzania, walikuwa wamekwama Tarakea kutokana na kufungwa kwa barabara hiyo.
“Huku tumekwama kusafiri kwa sababu barabara imefungwa kutokana na vurugu. Polisi wamelazimika kutumia nguvu kwa kurusha juu risasi za moto na kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao ambao baadhi wamejibu kwa kuwarushia mawe askari,”alisema Sanika
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi (ACP), Wilbroad Mutafungwa, alipotafutwa na Nipashe kwa njia ya simu alisema: “Niko njiani nakwenda Tarakea.
Kuna vurugu huko, lakini ni kweli Polisi wametumia nguvu ikiwamo mabomu ya machozi kwa ajili ya kuwatawanya wananchi hao waliofunga barabara. Naomba nitafute baadaye.”
Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki na Waendesha Bodaboda Wilaya ya Rombo, Abraham Urio, alisema eneo hilo lina changamoto ya kukosa vivuko vya watembea kwa miguu na matuta kwa ajili ya kukabiliana na magari yanayopita kwa mwendokasi mkubwa na hivyo kuna haja ya kurekebisha kasoro hiyo.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment