Serikali imesema itayatoza faini makampuni ya simu yaliyoshindwa kutimiza masharti ya mkataba walioingia na serikali wa kufikisha huduma za mawasiliano ya simu katika maeneo mbalimbali hasa vijijini chini ya mfuko wa mawasiliano kwa wote kwakuwa hali hiyo inaendelea kuchelewesha maendeleo kwa wananchi wa maeneo husika.
Akizungumza na viongozi wa idara mbalimbali za serikali pamoja na viongozi wa Chama cha Mapinduzi na serikali mkoani Iringa Waziri wa miundombinu mawasiliano na uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameyataja makampuni yaliyo kwenye hatari ya kukumbana na adhabu hiyo kuwa ni Halotel,Tigo,Vodacom na Airtel pamoja na kampuni ya serikali ya TTCL.
Mkuu wa mkoa wa Iringa Bi Amina Masenza amesema kampuni ya Halotel ilifika ofisini kwake kutaka kukabidhi moja ya miradi ya mawasiliano waliyopewa kujenga lakini kwakuwa kampuni hiyo haikuwa imetimiza masharti ya mkataba serikali ya mkoa ilikataa kupokea mradi huo.
Aidha mkuu huyo wa mkoa ameiomba serikali kupitia Wizara ya Miundombinu Mawasiliano na Uchukuzi kujenga kwa kiwango cha lami baadhi ya barabara ikiwemo barabara ya mchepuo ya Igumbilo Tumaini yenye urefu wa zaidi ya kilometa saba ili kupunguza msongamano wa magari kati kati ya mji wa Iringa kutokana na ongezeko la magari yanayotumia barabara ya Iringa Dodoma mara baada ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa zaidi ya kilometa 200 kukamilika .
Post a Comment