Loading...

HABARI YA KUSIKITISHA NA HII HAIJAWAHI KUTOKEA, MTOTO WA RAIS MSTAAFU JK (RIDHIWANI) ALIMWA BARUA NZITO BAADA YA KUGUNDULIKA KUWA NA DENI KUBWA KIASI HIKI

 WAKATI barua inayomtaka alipe deni la hoteli moja maarufu mkoani Arusha ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete, amefunguka na kusema ni mbinu za wapinzani wake kumchafua kisiasa.

Barua inayosambazwa kwa wiki nzima kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, ikiwa na Kumbukumbu Namba MDCAL/RK/05/2016, inaonyesha kuwa imetumwa kwenda kwa mbunge huyo Mei 27, mwaka huu ikimpa nafasi ya mwisho kulipa deni hilo kabla nguvu haijatumika.
Barua hiyo inaonyesha imetumwa na kampuni ya udadali wa kukusanya madeni ya Marcas Debt Collectors and Auctioneers (T).
Katika barua hiyo, Marcas kwa niaba ya hoteli hiyo ya Arusha, inamtaka Ridhiwani kulipa Sh. 891,600 kwa haraka baada ya kuzungusha malipo kwa miezi kadhaa sasa.
Alipotafutwa na Nipashe kwenye viwanja vya Bunge mwishoni mwa wiki, Ridhiwani alisema hatambui deni hilo la hoteli na kusisitiza kuwa kinachofanyika ni fitna za kisiasa.
"Hizo ni fitna za kisiasa tu. Watu wamekosa cha kusema, wameona wafanye hivyo. Mimi muda mwingi nakaa hapa Dodoma, nimekwenda lini huko Arusha?" Alihoji Ridhiwani.
Nipashe iliwatafuta maofisa wa kampuni iliyoandika barua hiyo iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ili kujua undani wa madai hayo lakini mtu aliyepokea simu alisema suala hilo lilishamalizika.
“Hapo hakuna habari yoyote ya kuandika ndugu yangu, kama unataka habari njoo tukupe habari, lakini hiyo ya Ridhiwani imesha expire (imepitwa na wakati),” alisema kupitia moja ya namba za simu zilizo kwenye barua huyo, mtu aliyekataa kujitambulisha jina licha ya kukiri kuwa ni mmoja wa maofisa wa Marcas.
Kwa tafsri isiyo rasmi, sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza inasema "Mteja wetu amekuita mara kwa mara ili kumalizana kuhusu deni hilo lakini umeshindwa kumlipa na hata huonyeshi nia ya kumlipa."
Katika barua hiyo, Marcas wanaeleza kuwa kutokana na kusababisha hasara kwa mteja wao, wameagizwa kuchukua hatua za kurejesha fedha anazodaiwa ikiwa ni pamoja na kuangalia mali zinazomilikiwa kwa jina la mbunge huyo.
Barua hiyo pia ilieleza kuwa Marcas wanamtaka Ridhiwani kulipa deni hilo kwa mkupuo ndani ya siku saba kuanzia Ijumaa iliyopita na kwamba vinginevyo watashikilia na kuuza mali yoyote anayoimiliki kisheria.
Barua hiyo imesaniwa na Bhoke Anderson, anayesomeka kuwa ndiye Mtawala Mkuu.
TAHADHARI YA RIDHIWANI
Desemba 27, mwaka jana, Ridhiwani aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutumia fursa hiyo kueleza upotoshaji unaoenezwa kuhusu yeye, hasa kuhusu mali na biashara zake.
Akifafanua, Ridhiwani alisema kuwa hana na wala hajawahi kumiliki lori au basi wakati wowote katika maisha yake.
Aidha, alisema hana hisa wala ubia na mtu yeyote au kampuni yoyote ya malori au mabasi.
"Nayasema haya kwa sababu wapo wabaya wangu wanaoeneza maneno ya kunihusisha na kumiliki malori na mabasi. Pia hunihusisha na baadhi ya makampuni yanayomiliki na kuendesha biashara ya malori na mabasi," alisema.
"Ndugu wanahabari, napenda kusema kwa kurudia na kusisitiza kuwa sina lori wala basi hata moja, na sina ubia na wafanyabiashara ama makampuni yoyote yanayofanya shughuli hizo.
"Kama yupo mtu yeyote ana ushahidi wa kuhusika kwangu auweke hadharani watu wauone. Napenda ieleweke kuwa kama ningekuwa na ubia wa namna hiyo nisingekuwa na sababu ya kuficha. Niogope kitu gani? Alisema Ridhiwani na kuongeza:
"Ukweli ni kwamba sizuiliwi kufanya biashara kama nikipenda kufanya hivyo. Hata kwa nafasi yangu ya sasa ya uongozi, yaani mbungen bado sina kizuizi.
Mbona bungeni wapo wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo? Isingekuwa ajabu kwangu kufanya biashara hivi sasa mimi pamoja na kuwa mbunge, ni mwanasheria wa kujitegemea na (kazi hiyo) nimeiweka katika tamko langu la mali na madeni la viongozi kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi (wa umma)."

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top