RAIS Mstaafu, Jakaya Kikwete ametajwa kukiuka Katiba kwa kutoa msamaha kwa watu waliotuhumiwa kwa kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ambao walikuwa hawajahukumiwa,anaandika Regina Mkonde.
Rais Kikwete ametajwa jana Bungeni mjini Dodoma na Khatibu Said Haji, Mbunge wa Konde wakati akiuliza swali la nyongeza kwa Harrison Mwakyembe, Waziri wa Katiba na Sheria baada ya kukanusha madai hayo yaliyosemwa na Haji.Mwakyembe alisema kuwa rais alikuwa sahihi kwa kuwa viko vifungu ambavyo vinampa nafasi hiyo.
“Kama ndiyo hivyo basi naomba ukubali kuwa Kikwete alivunja katiba ya nchi kwa kuwapa msamaha watuhumiwa wa EPA ambao walikuwa hawajahukumiwa bado, naomba majibu?” Alihoji Haji.
Kwenye swali la msingi Haji alitaka kujua kama rais kwa mujibu wa ibara ya 45(1) A mpaka D anayo mamlaka ya kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yeyote ambao mashauri yake yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi au upelelezi au mahakamani.
Katika utetezi wake Mwakyembe alijibu kuwa ibara hiyo inampa mamlaka rais ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote anayepatikana na hatia mbele ya mahakama kupitia kifungu cha kwanza.
“Kifungu cha pili kinampa rais mamlaka ya kumwachia kabisa au kwa muda maalum mtu yeyote aliyehukumiwa kuadhibiwa kwa kosa lolote,
na katika kifungu cha tatu rais anaweza badilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu kwa kosa lolote iwe adhabu tahafifu na kifungu cha nne anaweza kufuta adhabu yoyote au sehemu ya adhabu,”alisema Mwakyembe.
Alisema rais hawezi kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo mikononi mwa vyombo vya dola kwa kuwa hatma yao ipo kwenye mamlaka za mahakama, mashtaka na uchunguzi.
CHANZO: MWANAHALISIONLINE
Post a Comment