MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewapandisha kizimbani, mhariri na mwandishi wa gazeti la Dira ya Mtanzania, Musa Mkama na Prince Newton kwa kosa moja la kuandika habari za uongo zilizoleta mtafaruku kwa jamii, anaandika Josephat Isango
Akisoma hati ya mashtaka leo mbele ya Hakimu Respicius Mwijage, Wakili wa serikali, Timon Vitalis na Hellen Mushi, alidai mahakamani hapo kuwa, mnamo Juni 20 katika eneo la Biafra Kinondoni, Jijini Dar es Salaam washtakiwa hao waliandika na kuchapisha habari za uongo katika gazeti la ‘Dira ya Mtanzania’ toleo la 424 la tarehe 20 hadi 26 ambazo zilisababisha hofu na mshtuko kwa jamii kwa kutoa taarifa za uongo kuwa ’ Kifaru cha kivita cha Jeshi la Wananchi(JWTZ), chaibwa.
Amedai kuwa kitendo hicho ni kosa kisheria na ni kinyume na sheria ya magazeti.
Wakili Vitalis amedai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, washtakiwa hao wamekana shtaka hilo na Hakimu Mwijage amewataka kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh milioni 5.
Washtakiwa hao wamekidhi masharti ya dhamana na Hakimu Mwijage ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 5 mwaka huu itakapotajwa tena.
Hata hivyo, chapisho hilo hilo katika ukurasa wa mbele na wa pili lilichapa kwa maandishi makubwa meusi na mekundu taarifa iliyosema: ‘Mwakyembe atuhumiwa kutapeli Bil.2.’ ambayo yalimuudhi Harrison Mwakyembe, Waziri wa Katiba na Sheria.
Mwakyembe ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari Mjini Dodoma na kudaikuwa, chombo hicho kimekosa weledi na kimepotosha umma kutokana na chapisho hilo.
“Hii si mara yangu ya kwanza kutuhuma na baadhi ya habari kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kisiasa, napenda nikiri mbele yenu kuwa sijawahi, kushuhudia upotoshaji mkubwa na wa makusudi na uzushi uliopitiliza na chuki binafsi iliyo bayana kama ambavyo gazeti hili limefanya,” amsema Dk. Mwakyembe na kuongeza;
“Nina taarifa kuwa, wameuza sana magazeti; naambiwa print order (idadi ya nakala) yao imeongezeka na kwamba taarifa yao imesambaa kwenye mitandao ya jamii, hivyo dunia nzima inajua mimi nina tuhuma za wizi, za utapeli.”
Pia amesema, gazeti hilo lililendelea kuandika tena Juni 20 wiki hii kwa kuuthibitishia ulimwengu kuwa, “Dk. Mwakyembe ni tapeli na ushahidi wao mkubwa wametaja barua iliyowahi kuandikwa na Kampuni ya Power Pool mwaka 2010 na mimi kutumiwa nakala kwa mtanzdao (e-mail) wanayodai ni yangu. Kwa busara za gazeti hili, huo ni ushahidi tosha kuwa mimi ni tapeli.
“Gazeti hilo halina staha na miiko ya uandishi wa habari, kikosi chetu cha jeshi huko Kisarawe kilielezewa kama kikundi cha wahuni hivi kinachopiga wananchi hovyo hovyo, kinapiga risasi za moto hovyo hovyo hadi kumpiga mwananchi moja kiunoni.”
Wakati huo huo ametoa tahadhari kwa televisheni kutosoma magazeti yenye taarifa tata akitoa mfano wa habari zilizoandikwa na gazeti la Dira kwamba, kifari cha jeshi kimeibwa.
“Tutafungua kesi hii Mahakama Kuu ya Tanzania, tutawapa taarifa kila tunavyoendelea. Bado tunaangalia impact (athari) na kuhusika kwa vyombo vikubwa vya habari kama ITV na STAR TV kutangaza taarifa za magazeti tata bila uangalifu ili na wao tuwahusishe katika kesi hii,” amesema na kuongeza;
“Kesi hii, nina uhakika, itajenga msingi imara wa wajibu na uhuru wa vyombo vya habari Tanzania kwa muda mrefu ujao.”
Post a Comment