Watu wasiojulikana ambao walionekana wakiwa wamevaa kanzu na vitambaa vyeupe kichwani wamevamia maskani kuu ya CCM Kisonge na kulipua kontena kwa kutumia bomu la kutengezwa kienyeji, katika Mtaa wa Michezani mjini Zanzibar.
Mlipuko huo ulileta mtafaruku mkubwa kwa wakazi wa eneo zima la nyumba za Maendeleo Michenzani na mitaa ya karibu yake mjini hapa.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alitembelea eneo hilo na kusema kuwa vitendo vya hujuma havikubaliki wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa marudio wa Zanzibar.
Balozi Seif alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchaguzi wa kina wa tukio hilo, kuwasaka watu waliohusika na kuhakikisha wanafikishwa katika vyombo vya sheria Zanzibar.
“Nia ya Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuona wananchi wake wanaishi katika hali ya amani na utulivu,” alisema Balozi Seif.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam alithibitisha kutokea kwa mlipuko wa bomu hilo na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi kujua chanzo chake na waliohusika.
Alisema baada ya kutokea tukio hilo askari walifika na kuanza kufanya uchunguzi ikiwemo kuchukua mabaki ya mlipuko huo.
Shuhuda wa tukio hilo, Shaaban Said, ambaye ni mkazi wa eneo hilo, alisema aliona kikundi cha vijana wasiopungua sita waliovalia kanzu na vitambaa vyeupe kichwani wakiwa ndani ya gari ndogo aina ya Suzuki Carry, waliokuwa wakilizunguka kontena hilo.
“Dakika chache baadaye niliona wakiondoka kwa mwendo wa kasi na kisha tukasikia kishindo kizito," alisema Said na kueleza zaidi, "na kuna baadhi ya vioo vya madirisha ya nyumba za michenzani vilipasuka pasuka kwa kishindo hicho.”
Naye Mwajuma Seif Said, mkazi wa Michezani, alisema alisikia mlipuko huo na kuamua kukimbilia chooni akiwa na watoto wake.
“Nilipata wasiwasi sana nikiwa na watoto wangu," alisema Mwajuma. "Sikujua kilichokuwa kimetokea nje lakini baada ya muda nilianza kuona watu wakikusanyika mbele ya maskani ya Kisonge.”
Katibu wa Maskani ya CCM Kisonge, Mzee Yunus alisema mlipuko huo ulitokea baada ya kutegwa chini ya kontena ambalo hutumika kuhifadhi vifaa.
Alisema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa marudio serikali inapaswa kuimarisha ulinzi kwa usalama wa raia na mali zao.
Mzee alisema kuna baadhi ya mambo yanafanyika kwa chuki za kisiasa hivyo ni muhimu kwa serikali kuimarisha ulinzi katika maeneo ya huduma za umma, ili kupambana na watu wanaofanya vitendo hivyo.
Huu ni mlipuko wa tatu wa bomu lililotengenezwa kinyeji katika maeneo tofauti.
Pamekuwa na mlipuko katika eneo la Mkunazini na Michezani TAX tangu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 28 mwaka jana.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment