Loading...

Ukawa: CCM wanatuumiza

Charles Kuyeko, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala (Ukawa) (Wakwanza), Edward Lowassa, aliyekuwa Mgombea Urais kwa tiketi ya Ukawa na Boniface Jacob, Meya wa Halmashauri ya Kinondoni (Ukawa)VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vinalalamika kuhujumiwa na na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaandika Regina Mkonde.
Viongozi wa vyama hivyo wanaeleza kuwa, hujuma za kisiasa zinazoendelea kufanywa na baadhi ya viongozi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, zimeacha athari kubwa.
Na kwamba, hujuma hizo zimesababisha Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni kukosa msaada wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi.
Kauli hiyo imetolewa jana na Boniface Jacob (Chadema), Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Jacob amesema kuwa, hujuma hizo zinahusisha kuwazuia viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwenda safari za nje ya nchi ambazo zinalenga kukutana na wafadhili kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye wilaya zao.
“Hali ya kimahusiano kati ya mameya wanaotokana na Ukawa na Serikali Kuu si mazuri hata kidogo, viongozi tumeamua tuhabarishe umma wa Watanzania kuwa, kuna hujuma za waziwazi zinazofanywa na wenzetu juu ya shughuli za mameya wa Kinondoni, Ilala na Jiji la Dar es Salaam,” amesema.
Jacob amesema kuwa, hivi karibuni Ubalozi wa Uturuki ulidhamini safari ya mameya kwenda Uturuki kukutana na wadau na wafadhili wa miradi mbalimbali ikiwemo wa ujenzi wa Chuo Cha Ufundi ndani ya Manispaa ya Kinondoni.
“Ubalozi huo ulikuwa umeshatoa kibali cha kusafiri (Visa) na kugharamia fedha za usafiri, malazi, chakula na gharama zingine zote, ambapo matayarisho tu yali gharimu kiasi cha Dola za Marekani 42,000 (Sh 88 milioni) kwa mameya wote wanne, mtendaji mmoja mmoja kila halmashauri,” amesema.
Anasema, fedha hizo zililenga pia kugharamikia  mikutano iliyotakiwa kuanza tarehe 16 Juni mpaka 19 Juni 2016 na kwamba, wafadhili na wadau wa maendeleo waliandaa mialiko ya wawekezaji na wafadhili kutoka sehemu mbali mbali za Uturuki.
“Wafadhili hao walitarajiwa kuja Makao Makuu ya nchi hiyo, Jiji la Instanbul ili kukutana nasisi kujadili miradi ya maendeleo lakini serikali imevunja safari hiyo,” amesema.
Amesema, kitendo hicho cha serikali kuwazuia kimesababisha manispaa za Jiji la Dar es Salaam kukosa fursa za maendeleo ikiwemo chuo hicho cha ufundi.
“Si mara ya kwanza kwa sisi mameya kuhisi kuhujumiwa na baadhi ya viongozi serikalini ambao kimsingi, sisi tuliamini uchaguzi umeshapita na kwamba kila mmoja wetu atampa mwenzake heshima inayostahili juu ya ajenda za maendeleo,” amesema na kuongeza;
“Ndiyo maana kama nilivyo sema hapo awali, tumekuwa kimya juu ya vikwazo vidogo vidogo ambavyo tulihisi ni hujuma.
“Lakini tukaamua kuwa kimya na wavumilivu lakini tunatambua kuwa ipo mikakati ovu mingi dhidi yetu, ya kutukwamisha tusifanikiwe kuleta Maendeleo ndani ya mkoa wetu na wilaya zetu,” amesema.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top